Nini kilichoandikwa leo ndani ya magazeti ya Ujerumani
17 Novemba 2004Bibi Condoleezza Rice ameteuliwa kuwa waziri mpya wa mambo ya kigeni wa Marekani . Juu ya mada hiyo, gazeti la BERLINER TAGESSPIEGEL liliandika hivi:
+ Watu weusi wawili wanapokezana katika uongozi wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, na kwa mara ya pili, baada ya Bibi Madeleine Albrifght, kuna mwanamke sasa usoni mwa wizara hiyo. Hii inadhihirisha uwazi wa kitamaduni ulioko ndani ya timu ya Rais George Bush. Kama timu hiyo itajaribu kuwa karibu na Ulaya ni suali la kubishwa. Waziri aliyepita wa mambo ya kigeni, Colin Powell, alikuwa ni mtu aliyetaka Marekani ikaribiane na Ulaya kwa vile katika serekali hiyo ya Marekani yeye hasa alikuwa anazisuka siasa za kiliberali na kutaka nchi yake iwe na ushirikiano na nchi nyingine za dunia. Lakini Colin Powell hajaleta hatua muhimu ya kulipa uhai Bara kongwe la Ulaya. Vingine ndivyo itakavokuwa kwa Bibi Condoleezza Rice. Katika masomo yake alivutiwa na myahudi wa kutoka Cheki, Josef Korbel, baba wa Madeleine Albright, ambaye aliikimbia nchi yake baada ya majeshi ya Wanazi ya Hitler kuingia nchi hiyo. Hivyo,aliielekeza hamu ya masomo yake kwa Ulaya ya Kati na Mashariki. Pale baba yake George Bush alipokuwa rais, Bibi Rice aliiongoza idara ya masuala ya Ulaya Mashariki katika Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani, na alishiriki katika yale mazungumzio baina ya sehemu mbili za iliokuwa Ujerumani na madola manne, Marekani, Uengereza, Ufaransa na Urussi ambayo yalipelekea kuungana tena Ujerumani.+
ALLGEMEINE ZEITUNG la mjini Mainz lilijishughulisha na suala na msimamo wa kisiasa wa siku za mbele wa waziri huyo mpya wa mambo ya kigeni wa Marekani:
+ Haibishwi kwamba Bibi Rice anawakilisha msimamo mkali, hivyo kuutilia nguvu ule msimamo mkali wa waziri wa ulinzi, Donald Rumsfeld. Suali kama kutakuweko na mabadiliko ya njia ya kisiasa itakayofuatwa ni jambo la kuwaza juu juu tu. Bibi Rice, kama mshuari wa usalama wa taifa na msiri mkubwa wa Rais Bush, amebeba dhamana ya maamuzi yote muhimu yaliochukuliwa katika mhula wa kwanza wa utawala wa Rais Bush, vikiwemo vita dhidi ya Saadam Hussein wa Iraq.+
Tubadilishe dira ya mazungumzo.
Wahariri wa magazeti wenye ndimi kali walipata kitu cha kuandika, nacho ni ripoti iliotolewa na ofisi ya kuchunguza hesabu za matumizi ya serekali ya Ujerumani.
Tunasoma hivi kutoka gazeti la DIE WELT kuhusu malalamiko yalioelezewa na idara ya kuchunguza hesabu za matumizi ya serekali ya Ujerumani:
+Hali ni mbaya sana, hata mtu anashindwa kupumua. Hali ni mbaya zaidi kuhusu bajeti, kuliko vile ilivoelezewa na mkuu wa idara hiyo, Dieter Engels. Siasa ya feha na ya kukopa inayoendeshwa na serekali ya Shirikisho ni haina dhamana. Fedha zaidi zinatumiwa kwa huduma za kijamii, ikiwa pamoja na riba ya fedha hizo. Kwa ajili ya uwekezaji wenye maana hakuna fedha zilizobakia, na vizazi vijavyo ambavyo vitakabiliwa na madeni hayo, havitakuwa na chochote cha kujivunia kutokana na uwekezaji unaofikiriwa vibaya na serekali.+
Gazeti la KÖLNER EXPRESS lilitoa tathmini ifutayo juu ya waziri wa fedha, Hans Eichel:
+ Idara ya kuchunguza hesabu za matumizi ya serekali ina maneno ya kumwambia mkopaji nambari moja, yaani waziri wa fedha wa serekali ya Ujerumani. Idara hiyo inamuumbua kabisa waziri Hans Eichel. Hatua kwa hatua idara hiyo inamlaumu mlinzi huyo wa hazina ya serekali, ikitaja orodha ndefu ya makosa anayoyafanya na anavozorotesha mambo. Kutokana na mambo kuwekwa wazi, ukosefu wa uwezo wa kisiasa wa waziri Hans Eichel ni mrefu zaidi na maafa ya kisiasa anayoyasababisha yanazidi kuwa mabaya siku hadi siku.Maji yamemfika hadi shingoni waziri huyo wa fedha.+
Majadiliano juu ya ushirikiano wa wakilishi wa wafanya kazi na waajiri katika kuamuwa mustakbali wa viwanda ni jambo lililozungumziwa na na gazeti la NEUE DEUTSCHLAND.
+Bila ya kuweko sababu inayoonekana, lakini hoja kali sana zikitumiwa, hivi sasa kuna mabishano juu ya suala la kukaa pamoja wawakilishi wa wafanya kazi na waajiri katika kuamuwa mustakbali wa viwanda. Hakutafanyika kitu, kwa vile ule wingi unaohitajika unakosekana. Hivyo, kwanini kuna makelele haya?
Mtu anaweza kuchukulia kwamba serekali imetaka kuwakasirisha waajiri. Na ikiwa kuna upande utakaofaidika na hii sarakasi ya majadiliano kuhusu kukaa pamoja wawakilishi wa wafanya kazi na waajiri, basi upande huo ni serekali hii inayoongozwa na vyama vya SPD na Kijani. Kwani bila ya kuuliza lini na vipi itakavogharimu, serekali itaweza tena kuvisaidia vyama vya wafanya kazi.+
Mchango wa vyama vya wafanya kazi umemulikwa na gazeti la HANDELSBLATT linalochapishwa Düsseldorf:
+ Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanya kazi la hapa Ujerumani, DGB, Bwana Michael Sommer, hivi sasa anajionea machipuko ya pili ya kisiasa. Tangu yalipoanza majadiliano juu ya kukaa pamoja wawakilishi wa wafanya kazi na waajiri katika kuamua hatima za viwanda, Shirikihso hilo la wafanya kazi sasa liko katika hali nzuri. Katika mapambano ya kupata kauli katika mabaraza ya kusimamia viwanda kwa ajili ya wanaharakti wa Chama cha wafanya kazi wa viwanda vya vyuma na wale wa huduma za umma, vyama vya wafanya kazi na chama tawala cha SPD viko bega kwa bega. Kansela wa Ujerumani, ambaye hadi karibuni alikuwa analaumiwa na watu wa mrengo wa shoto katika maandamano ya kuupinga Mpango wa Hartz kuwa ni mhaini wa wafanya kazi, hivi sasa anasonga mbele kwa nguvu.+
Miraji Othman