Nigeria: Wanajeshi wauliwa na wapiganaji wa kundi la IS
4 Mei 2025Vyanzo vya kijeshi nchini humo vimesema, mauaji hayo yametokea baada ya wapiganaji wa IS wa eneo la Afrika Magharibi (ISWAP) kuishambulia kambi ya jeshi iliyopo katika mji wa Buni Gari, ulio kilomita 60 kutoka Damaturu, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Yobe.
Huenda idadi ya wanajeshi waliouawa ikaongezeka kwa sababu baadhi ya wanajeshi bado hawajulikani walipo. Kambi hiyo imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara na wapiganaji wa itikadi kali za kidini.
Vyanzo vya kijeshi ambavyo havikutaka kutambulishwa vimesema washambuliaji hao wa IS walipora silaha na kisha waliichoma kambi hiyo, ambako magari na majengo kadhaa ya kijeshi yaliteketea. Uasi huo uliodumu kwa muda wa miaka 16 umegharimu maisha ya zaidi ya watu 40,000 na kuwalazimisha takriban watu milioni mbili katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria kuyakimbia makazi yao.