Niger yaanza uchimbaji madini ya shaba ili kutanua mapato
24 Februari 2025Niger imetangaza jana kukaribia kuanza kwa uchimbaji wa madini ya shaba katika eneo lake la jangwa la kaskazini wakati nchi hiyo ikijaribu kupanua vyanzo vyake vya rasilimali.
Niger, ambayo tayari ni mzalishaji mkubwa wa madini ya Uranium, imetoa kibali kwa kampuni ya taifa ya Compagnie Miniere de l'Air (Cominair SA) katika eneo la Agadez, kulingana na taarifa ya baraza la Mawaziri iliyoonwa na shirika la Habari la AFP
Serikali ya kijeshi iliyochukua mamlaka katika mapinduzi ya mwezi Julai mwaka 2023, ilisema utafiti ulionyesha kuwa migodi hiyo inaweza kuzalisha tani 2,700 kwa mwaka kwa muongo mmoja, na kutengeneza ajira za moja kwa moja 300 na kuzalisha mapato ya mamilioni ya dola kwa serikali.
Tangu kuchukua madaraka, utawala wa kijeshi umejaribu kuchukua udhibiti wa shughuli za uchimbaji madini, kuondoa kibali cha uchimbaji wa madini ya lithiamu kwa kampuni ya Ufaransa ya Orano, ambayo imekuwepo katika koloni la zamani la Ufaransa kwa miaka 50.