Niger, Mali na Burkina Faso zaiaga rasmi ECOWAS
29 Januari 2025
Kuondoka kwa mataifa hayo matatu katika Jumuiya hiyo ya ECOWAS kulikotangazwa kwa mara ya kwanza mwaka mmoja uliyopita, kumeanza kutekelezwa rasmi hii leo, hii ikiwa ni kulingana na taarifa kutoka Jumuiya hiyo, Lakini ikasema kuwa imeiwacha milango yake wazi, huku ikitoa wito kwa nchi wanachama kuendelea kutoa huduma za kiuanachama kwa mataifa hayo matatu ikiwemo uhuru wa kusafiri ndani ya kanda hiyo kwa kutumia paspoti ya ECOWAS, kufanya biashara na kuendelea na ushirikiano wa kidiplomasia na mataifa mengine.
Mataifa ya Sahel kuunda muungano wa kupambana na wanamgambo wa kijihadi
Niger Mali na Burkina Faso zimeondoka katika Jumuiya hiyo, licha ya juhudi kadhaa za kutaka mataifa hayo kuendelea kuwa wanawachama. Hii inamaanisha takriban watu milioni 73 wanaondoka katika moja ya Jumuiya kubwa barani Afrika, iliyokuwa na wanachama 15 iliyo na nia ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa wanachama ili kuimarisha hali ya maisha.
Mataifa hayo matatu sasa yameunda muungano wao wa ulinzi wa mataifa ya sahel AES na kuanzisha pia paspoti zao za pamoja. Eneo la Sahel limekuwa likikabiliwa na mashambulizi ya wapiganaji walio na itikadi kali kwa miaka kadhaa sasa na mataifa hayo matatu yameituhumu Ufaransa kushindwa kudhibiti hali.
Mapinduzi ya kijeshi yaharibu mahusiano ya mataifa hayo na ECOWAS
Mahusiano kati ya mataifa hayo matatu na Jumuiya hiyo yaliingia doa tangu kulipotokea mapinduzi ya kijeshi nchini Mali mwaka 2021, Burkina Faso 2022 na Niger 2023. Bamako, Ouagadougou and Niamey zinaishutumu ECOWAS, ambayo iliyakosoa mapinduzi hayo na kutangaza vikwazo dhidi ya mataifa hayo kwa kushawishiwa na Ufaransa koloni lao la zamani. Kwa sasa mataifa hayo matatu yanasemekana kujisogeza karibu zaidi na Urusi.
ECOWAS yasikitishwa kukosekana muafaka na serikali za kijeshi
Mataifa hayo yanawakilisha asilimia 17 ya idadi jumla ya watu milioni 440 katika kanda hiyo na zinachangia pia asilimia 8 ya pato la pamoja la kiuchumi. Mali, Niger na Burkina Faso ni miongoni mwa mataifa 10 zilizo na maendeleo madogo sana duniani licha ya rasilimali kubwa ilizonazo kama dhahabu na urani ambazo mara kwa mara huchimbwa na makampuni ya Ulaya na Amerika ya kaskazini.
Barabara zinazopitia nchi hizo tatu zinatumiwa kwa ulanguzi wa madawa na biashara haramu ya kusafirisha binaadamu kufika Ulaya, na mataifa hayo pia kwa sasa yanapambana na makundi ya kikaidi.
Reuters, afp, ap