NEW YORK : Onyo juu ya ufukara wa Afghanistan
22 Februari 2005Repoti ya Umoja wa Mataifa kwa Afghanistan imebainisha kwamba matatizo mazito ya kijamii na elimu yanaendelea kubakia nchini humo miaka mitatu baada ya kupinduliwa kwa utawala wa Taliban na vikosi vya Marekani.
Uchunguzi wa msaada wa maendeleo wa Umoja wa Mataifa umegunduwa kwamba wananchi wa Afghanistan bado ingali wana kiwango kikubwa sana cha watu wasiojuwa kusoma na kuandika, watu kutoishi muda mrefu na kiwango kikubwa cha vifo vya watoto. Tokea kupinduliwa kwa utawala wa Taliban uchumi wa Afghanistan umekuwa kwa asilimia 25 kwa kiasi kikubwa kutokana na uzalishaji wa zao la kasumba lakini wananchi mafukara wa nchi hiyo wamekuwa na kipato kidogo.
Repoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imeonya kwamba iwapo hali hiyo itaachiliwa bila ya kutafutiwa ufumbuzi Afghanistan inaweza kutumbukia tena katika machafuko.
SEOUL : Korea Kaskazini kurudi katika mazungumzo
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-il amemweleza mjumbe wa China kwamba nchi yake itarejea kwenye mazungumzo ya nuklea ya nchi sita iwapo mazingira ya kufanya hivyo yatakuwa sahihi na Marekani kuonyesha uaminifu.
Hiyo ni taarifa ya kwanza kutolewa na kiongozi huyo tokea Korea Kaskazini kutangaza hadharani kwa mara ya kwanza mwezi huu kwamba ina silaha za nuklea na inajitowa kwenye mazungumzo yenye kuzishirikisha Korea Kusini,China,Russia,Marekani na Japani juu ya mpango wake wa nuklea.
Shirika la habari la serikali nchini Korea Kaskazini la KCNA limemkariri Kim akimwambia Wang Jiarui mkuu wa idara ya ushirikiano ya Chama cha Kikomunisti cha China kwamba watakwenda kwenye meza ya mazungumzo wakati wowote ule iwapo kutakuwepo na mazingira yaliyokomaa kwa ajili ya mazungumzo hayo kutokana na juhudi za pamoja za nchi husika kwa ajili ya kipindi cha usoni.