New York. Mataifa ya Ulaya yaipongeza Afghanistan.
19 Septemba 2005Umoja wa mataifa na mataifa kadha ya Ulaya yameipongeza Afghanistan kwa kufanya uchaguzi wake wa kwanza katika muda wa zaidi ya miongo mitatu.
Mkuu wa NATO Jaap de Hoop Scheffer amesema mamilioni ya watu, wake kwa waume wameweza kupiga kura bila matatizo na kidemokrasia.
Ameongeza kuwa NATO itaendelea kufanikisha ujenzi mpya wa nchi hiyo.
Kura hiyo imefanyika huku kukiwa na ulinzi mkali ambapo wanajeshi 100,000 wa Afghanistan na wale wa kimataifa wakilinda vituo mbali mbali vya kupigia kura.
Watu 11 wameripotiwa kuuwawa na wapiganaji wa Taliban.
Idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura inasemekana kuwa ni asilimia 50, ikiwa ni idadi ndogo kuliko waliojitokeza katika uchaguzi wa rais mwaka jana.