NEW YORK : Iran yagoma kutelekeza shughuli za nuklea
4 Mei 2005Iran imesema haitotelekeza shughuli yake ya nishati ya nuklea kama hakikisho dhidi ya hofu kwamba yumkini ikatengeneza silaha za nuklea wakati mataifa kadhaa yalipokuwa yakizungumza hapo jana juu ya haki ya kuwa na teknolojia ya atomu kwa ajili ya amani katika mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya Mkataba wa Kuzuwiya Kuenea kwa Silaha za Nuklea.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Kamal Kharazi amesema Iran kwa upande wake imeazimia kutumia nyanja zote za halali za teknolojia ya nuklea ikiwa ni pamoja na kurutubisha uranium mahsusi kwa dhamira za amani.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Yoschka Fischer ameonya hapo Jumatatu kwamba Iran kuanza tena kurutubisha uranium kutakuja kupelekea kusambaratika kwa mazungumzo na Umoja wa Ulaya yenye kuitaka nchi hiyo itowe hakikisho kwamba haitengenezi mabomu ya nuklea.
Fischer pia amesema kushindwa kufikiwa kwa suluhisho katika mazungumzo hayo pia kutapelekea shinikizo la Umoja wa Ulaya na Marekani ambayo ambayo inadai kwamba Iran inatengeneza kwa siri silaha za nuklea kuifikisha nchi hiyo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuangalia uwezekano wa kuiwekewa vikwazo vya kimataifa.