NEW YORK : Ahmedinejad ashutumu Marekani na Uingereza
20 Septemba 2006Mjini New York Rais Mahmoud Ahmedinejad wa Iran amehutubia kikao cha 61 cha Baraza Kuu la Umoja.
Katika hotuba yake ameishutumu Marekani na Uingereza kwa kuwa mataifa yenye kudhoofisha kuaminika kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na uwezo wake wa kufanya kazi kwa ufanisi. Pia amesisitiza kwamba mpango wa nuklea wa Iran ni kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi tu.Ahmedinejad pia ameishutumu Marekani kwa kuendesha vita nchini Iraq na Israel kwa kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.
Akizungumza katika Baraza hilo Kuu la Umoja wa Mataifa Rais George W. Bush wa Marekani amewashutumu watawala wa Iran kwa kuponda utajiri wa nchi hiyo kugharamia ugaidi na utafiti wa silaha za nuklea hata hivyo amesema yuko tayari kutumia zaidi diplomasia kabla ya kuchukuwa hatua za kuiwekea vikwazo nchi hiyo.
Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilifunguliwa na Katibu Mkuu wa Umoja huo Kofi Annan ambaye ilikuwa ni mara yake ya mwisho kufanya hivyo.Annan anatarajiwa kun’gatuka hapo mwezi wa Desemba baada ya kutumika kwa vipindi viwili vya miaka mitano kama mkuu wa chombo hicho cha dunia.