New Orleans, Marekani. Waokoaji na waliofariki wakumbukwa.
30 Agosti 2006Mji wa mashariki wa New Orleans nchini Marekani umeadhimisha mwaka mmoja tangu maafa yaliyosababishwa na kimbunga Katrina kwa kutoa shukrani kwa waokoaji na wale waliouwawa na kimbunga hicho.
Rais wa Marekani George W. Bush alishiriki katika misa ya kuwaombea wafu mjini humo.
Amesema kuwa anachukua dhamana kamili kutokana na kushindwa kwa serikali kuu kuchukua hatua za haraka na kuahidi kufanya vizuri mara nyingine kunapotokea maafa kama hayo.
Kwa mujibu wa kituo cha taifa la kupambana na maafa ya vimbunga , Katrina kimeuwa zaidi ya watu 1,500 katika majimbo manne, na maeneo ambayo yameathirika sana yakiwa ni Luoisiana na Mississippi.
Wakati huo huo kimbunga cha maeneo ya tropiki kinachojulikana kama Ernesto kinatarajiwa kulikumba eneo la Florida katika muda mfupi ujao.
Kimbunga hicho kwa muda kilipata nguvu jana Jumapili, kabla ya kupoteza tena nguvu zake wakati kikipita katika maeneo ya milima katika kisiwa cha Cuba.