Neuer kukosa mechi mbili za Bundesliga
24 Machi 2025Kipa wa Bayern Munich Manuel Neuer atakosa mechi mbili za Bundesliga kutokana na jeraha na haijabainika wazi ikiwa atakuwa amepona na kuwa "fiti" vya kutosha kucheza mechi ya duru ya kwanza ya robo fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya, Champions dhidi ya Inter Milan.
Vyombo vya habari likiwemo jarida la michezo la Kicker na televisheni ya Sky vimesema Neuer alichanika msuli wa nyuma ya mfupi wa mguuni wakati wa mazoezi wiki iliyopita katika jitihada ya kurejea mchumani baada ya kupata jeraha kama hilo zaidi ya wiki mbili zilizopita katika mechi ya ligi ya mabingwa dhidi ya Bayer Leverkusen.
Bayern wamesema siku ya Jumamosi kwamba Neuer atachukua mapumziko mengine kutoka kwa mazoezi katika siku zijazo kufuatia jeraha hilo jipya.
Ripoti zilizotolewa siku ya Jumapili zilisema atakosa mechi za Bundesliga dhidi ya St Pauli nyumbani Allianz Arena Machi 29 na ugenini dhidi ya Augsburg siku sita baadaye.
Bayern Munich watakuwa na miadi na Inter Aprili 8, huku duru ya marudiano ikichezwa mjini Milan Aprili 16. Ripoti zinasema siku zijazo zitaamua ikiwa Neuer, ambaye atafikisha miaka 39 ya kuzaliwa Alhamisi ijayo, atakuwa pia katika mashaka ya kucheza mechi dhidi ya Inter.
Kipa mpya aliyesaliwa Januari mwaka huu Jonas Urbig amekuwa akisimama mchumani kuchukua nafasi ya Neuer katika mechi tatu za ligi na anapewa nafasi kubwa kusimama tena katika lango.
Makipa wengine wa Bayern ni Daniel Peretz na Sven Ulreich, ambao wote wamewahi kushikilia nafasi ya Neuer msimu huu.