Netanyahu ziarani nchini Hungary akaidi amri ya ICC
3 Aprili 2025Netanyahu alikaribishwa kwa gwaride la kijeshi na kulakiwa na mwenyeji wake Waziri Mkuu wa Hungari na mshirika wake wa karibu, Viktor Orban.
Viongozi hao wawili watafanya mazungumzo baadaye leo, na Netanyahu pia anatarajiwa kukutana na Rais Tamas Sulyok, wa Hungari katika Kasri ya lake mjini Budapest. Hii ni ziara ya pili ya Netanyahu nje ya Israel tangu ICC ilipotoa waranti wa kukamatwa kwake mnamo mwezi Novemba.
Kufuatia ziara hiyo ya Netanyahu serikali ya Hungary imetangaza rasmi kuanza mchakato ya kujiondoa uanachama wake katika mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC, iliyotoa waranti hiyo.
Mkuu wa Wafanyakazi katika serikali ya Orban Gergely Gulyás aliandika katika mtandao wa X kwamba mchakato huo utaanza mara moja, kutoka katika chombo hicho cha juu cha haki.
Hungary yajiondoa ICC ni kupinga kukamatwa kwa Netanyahu
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, yenye makao yake The Hague, Uholanzi, ilisema ilipotoa hati yake kuwa kuna sababu za kuamini kuwa Netanyahu na waziri wa zamani wa ulinzi wa Israeli, Yoav Gallant, walitumia “njaa kama mbinu ya kivita” kwa kuzuia misaada ya kibinadamu Ukanda wa Gaza na walilenga raia kwa makusudi katika kampeni yake dhidi ya Hamas – mashtaka ambayo maafisa wa Israeli imekanusha.
Baada ya ICC kutoa hati hiyo mnamo Novemba, Orban alishutumu mahakama hiyo, akidai kuwa ni chombo pekee cha kimataifa cha kudumu cha kushughulikia uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari lakini “kinajiingiza katika mzozo unaoendelea kwa sababu za kisiasa,” akisema hatua hiyo inadhoofisha sheria za kimataifa na kuongeza mivutano.
Mwaliko wake kwa Netanyahu ulikuwa hatua ya wazi ya kupinga uamuzi wa mahakama hiyo. Hungary ilijiunga na ICC mwaka 2001, wakati wa muhula wa kwanza wa Orbán kama waziri mkuu.
Soma pia:Hungary yajiondoa kutoka mahakama ya ICC
Kwa sasa, nchi zote 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya, ikiwemo Hungary, ni wanachama wa ICC, na wanawajibika kumkamata mtuhumiwa yeyote mwenye waranti ya kukamatwa endapo ataingia katika nchi zao. Hata hivyo, mahakama hiyo inategemea nchi wanachama kutekeleza maagizo yake.
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu imeikosoa Hungary kwa kukaidi waranti wa kukamatwa kwa Netanyahu.
Msemaji wa mahakama hiyo, Fadi El Abdallah, amesema si wajibu wa nchi wanachama kuamua kwa hiari uhalali wa maamuzi ya mahakama hiyo. “Hungary bado ina jukumu la kushirikiana na ICC,” alisema.
Israel yapongeza uamuzi wa Hungary
Baada ya uamuzi wa Hungary kutangaza kujiondoa kutoka ICC, Waziri wa Mambo ya Nje Israeli, Gideon Saar, amempongeza Orban kwa hatua hiyo ya kujiondoa ICC
“Ninaipongeza Hungary kwa uamuzi wake muhimu wa kujiondoa kutoka ICC.” Aliandika katika mtandao wa X.
Aliongeza kwamba hatua hiyo ya Hungary inaonesha uungaji mkono wa wazi kwa Israel pamoja na misingi ya haki na uhuru wa kitaifa.
Wakati hayo yakiendelea Mamlaka ya Palestina iliitolea mwito Hungary wa kumkamata Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anayezuru nchini humo.
""Wizara inatoa wito kwa serikali ya Hungary... kutekeleza agizo la kukamatwa Netanyahu na kumkabidhi mara moja kwa ICC ili kumfikisha mbele ya sheria." Ilisema sehemu ya taarifa ya Wiazara ya Mambo ya Nje ya Mamlaka Palestina.
Mashambulizi Gaza yauwa watu zaidi ya hamsini
Kwa mujibu wa duru za hospitali, watu wasiopungua 50 wameuawa kwenye mashambulio ya Israel ya usiku kucha katika ukanda wa Gaza. Kulingana na taarifa rasmi kutokea Khan Younis iliyo kusini mwa Ukanda huo,maiti za watu 14 zilipelekwa hospitali ya Nasser, tisa zikiwa za familia moja. Watoto watano na wanawake 4 ni baadhi ya waliouawa.
Maiti nyengine 19 zikiwemo za watoto na mama mjamzito zilipelekwa kwenye hospitali ya Ulaya iliyoko karibu na Khan Younis.Mjini Gaza kwenyewe,maiti 21 zilipelekwa kwenye hospitali ya Ahli.
Wakaazi wa maeneo ya Shujaiya,Jadida,Turkomen na mashariki mwa Zeytoun wameamriwa kuondoka na kwenda kwenye sehemu salama za magharibi mwa mji wa Gaza, kwani jeshi la Israel linajiandaa kwa mashambulizi mazito.
Haya yanajiri ikiwa ni siku moja baada ya Israel kubainisha kuwa itadhibiti maeneo makubwa ya Gaza na kufungua njia mpya salama itakayopitia eneo la himaya ya Palestina.
Soma pia:Israel yasema jeshi lake linapanua operesheni zake Gaza
Dhamira ni kulishinikiza kundi la Hamas na kulibinya eneo la mji wa Rafah lililo kusini. Umoja wa mataifa kupitia msemaji wake Stephane Dujarric umetahadharisha kuhusu hatua hiyo ya kutenga njia mpya.
"Katibu Mkuu anakumbusha kuwa azimio la baraza la usalama la Umoja wa mataifa la 2735 linapinga juhudi zozote za kubadili mipaka ya Ukanda wa Gaza, ikiwemo hatua ya kupunguza ukubwa wake.
Kutokana na hilo,anatiwa wasiwasi na kauli za utengano za Israel akisema "Israel kujipanulia mipaka yake itakayoliongeza eneo la taifa lake:mwisho wa kumnukuu.Katibu Mkuu anausisitizia wito wake wa kudumisha makubaliano ya kusitisha vita.”
Kwa upande wake,Mamlaka ya Palestinainayoungwa mkono na mataifa ya magharibi iliyo pia mahasimu wa Hamas,imepinga hatua ya Israel ya kutenga njia mpya. Kadhalika imelitolea wito kundi la Hamas kuachia ngazi Gaza.
Yote hayo yakiendelea,Israel imeishambulia miji 5 ya Syria . Kitendo hicho kimezua wasiwasi na kitaathiri juhudi za muda mrefu za ustawi wa taifa hilo lililozongwa na vita wanaeleza wachambuzi.