Israel yaapa kulipa kisasi dhidi ya Wahouthi
5 Mei 2025Katika ujumbe wa maneno na baadaye kupitia mtandao wa kijamii wa X, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema nchi yake itajibu shambulizi la Wahouthi lililoulenga uwanja wa ndege wa Ben Gurion jana Jumapili.
Watu wanane walijeruhiwa pale waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran walipofyetua kombora la masafa kuulenga uwanja huo wa ndege uliopo maili chache kutoka mji wa Tel Aviv.
Safari za ndege zilizuiwa kwa muda mfupi na mashirika kadhaa ya Ulaya yalizifuta kabisa safari za kwenda Israel jana Jumapili.
Ripoti za vyombo vya habari vya Israel vilisema mifumo yote ya ulinzi wa anga ya Israel ikiwemo ule mamboleo kabisa kutoka Marekani wa THAAD, ilishindwa kulidungua kombora hilo lililosafiri kiasi umbali wa maili 2000 kutokea Yemen,
Netanyahu: Hatutavumilia mashambulizi ya Wahouthi
Kufuatia shambulizi hilo ambalo ndiyo la hivi karibuni kabisa kufanywa na waasi wa Houthi, Waziri Mkuu Netanyahu ameapa kuwa nchi yake itajibu, siyo kwa kuwalenga tu waasi hao bali pia Iran aloitaja kuwa "mfadhili mkuu wa ugaidi".
"Bila shaka tunajaribiwa, ulimwengu mzima unapimwa ubavu na Wahouthi, ikiwemo kwa shambulizi hili la kinyama walilolifanya karibu na uwanja wa Ben-Gurion. Hatutavumilia hilo. Tutachukua hatua kali dhidi yao na mara zote tutakumbuka kuwa wanafanya haya kwa msaada na mwongozo wa mfadhili wao Iran. Tutafanya lolote tunaloweza kulinda usalama wetu na kujibu kikamilifu na kuipa onyo la uhakika Iran kuwa haya hayawezi kuendelea". amesema Netanyahu.
Kwa miezi kadhaa sasa waasi wa Houthi wamekuwa wakifyetua makombora kuilenga Israel, wakisema wanafanya hivyo kuwaunga mkono Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Israel imejibu mara kadhaa kwa kuyapiga maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi na kwa wiki chache zilizopita jukumu hilo linafanywa na Marekani.
Mtandao wa habari nchini Israel wa ynet umeripoti kwamba mkutano wa dharura wa usalama ulioitishwa na Waziri Mkuu Netanyahu umeamua kwamba Israel itachukua hatua za kijeshi dhidi ya Wahouthi kwa kushirikiana kwa karibu na Marekani.
Israel yapanga kutanua operesheni ya kijeshi Ukanda wa Gaza
Katika hatua nyingine vyombo vya habari nchini Israel vimeripoti kuwa Baraza la Mawarizi lililoketi jana chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu limeridhia kutanuliwa kwa operesheni ya kijeshi kwenye Ukanda wa Gaza.
Vyanzo kadhaa vya ngazi ya juu vimekaririwa vikisema mpango huo utaanza kutekelezwa baada ya kumalizika kwa ziara ya Rais Donald Trump kwenye kanda ya Mashariki ya Kati wiki inayokuja.
Taarifa hizo zimefuatiwa na tangazo la Mkuu wa Majeshi wa Israel, Jenerali Eyal Zamir aliyesema serikali imeamuru kuitwa kazini mamia kwa maelfu ya askari wa akiba kwa dhima ya kuimarisha na kutanua operesheni ya kijeshi ya Israel huko Ukanda wa Gaza.
Akizungumza akiwa kwenye ziara ya kuitembelea kambi moja ya kijeshi kwenye mji wa Haifa, Jenerali Zamiri amesema wanalenga kuongeza mbinyo kwa kundi la Hamas ili iwarejeshe nyumbani mateka wa Israel inaowashikilia.
Ameapa kwamba awamu hiyo ijayo italisambaratisha kabisa kundi hilo na kuharibu miundumbinu yake yote ya juu na chini ya ardhi.
Vyanzo vya kuaminika vimearifu kwamba Waziri Mkuu Netanyahu amekwishatoa ruhusa kwa jeshi kutekeleza mipango yake.
Mapendekezo ya Israel kuhusu usimamizi wa misaada ya kiutu Gaza yapingwa
Wakati huo huo duru zinasema serikali ya Israel imeidhinisha mpango mpya wa kuruhusukupelekwa tena misaada ya kiutu kwenye ardhi ya Wapalestinalakini chini ya masharti ambayo Umoja wa Mataifa umeyapinga.
Chini ya mpango huo mpya, Israel inataka kubadilisha kabisa mfumo wote wa kusambaza mahitaji kwa dhamira ya kuondoa uwezekano kwa kundi la Hamas kuipoka misaada hiyo na kuielekeza kwa wapiganaji wake.
Sehemu ya mapendekezo yanataka Umoja wa Mataifa uwe na jukumu la kuidhinisha usambazaji misaada lakini chini ya usimamizi mkali wa jeshi la Israel.
Hata hivyo umoja huo umesema masharti hayo yatakwenda kinyume na misingi ya utoaji misaada ya kibanadamu kwa sababu Israel itakuwa na uamuzi wa mwisho wa kuamua mahali na wale wanapaswa kupewa misaada hiyo.
Umoja wa Mataifa umeonya kwamba sharti hilo linalenga kuipatia nguvu zaidi Israel kutumia misaada ya kiutu kama mkakati wa kijeshi na shinikizo kwa watu Gaza.