Netanyahu: Tutabadili sura ya Mashariki ya Kati
17 Juni 2025Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesisitiza kwamba kampeni yake dhidi ya Iran "itabadili sura ya Mashariki ya Kati", wakati nchi hizo mbili zikiendelea kushambuliana vikali kwa siku ya tano.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu jioni, Netanyahu alisema kuwa Israel inawaondoa viongozi wa kiusalama wa Iran "mmoja baada ya mwingine" na kwamba kwa kufanya hivyo wanabadili "sura ya Mashariki ya Kati, na hilo litaleta mabadiliko makubwa ndani ya Iran yenyewe".
"Tumeua safu ya juu ya viongozi wa usalama wa Iran, wakiwemo wakuu watatu wa kijeshi. Kamanda wao wa jeshi la anga, wakuu wawili wa kijasusi. Jana, tulimuua mwingine wa jeshi na jeshi la walinzi wa Mapinduzi. Tulimlenga mkuu wa kitengo chao cha operesheni. Tunamwondoa mmoja baada ya mwingine," alisema Netanyahu.
Wakati Netanyahu akitoa kauli hizo, Iran nayo imeendelea kuvurumusha makombora dhidi ya Israel, huku Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran likijigamba kwamba mashambulizi yataendelea "bila kukatizwa hadi alfajiri."
Hapo awali, matangazo ya moja kwa moja ya Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) yalikatizwa wakati shambulio la Israel lilipopiga jengo la shirika hilo mjini Tehran. Mtangazaji aliyekuwa mubashara alilazimika kukimbia kufuatia mlipuko mkubwa na kusababisha tishio la Iran la kulipiza kisasi dhidi ya vituo vya habari vya Israel.
Muda mfupi baada ya shambulio, matangazo yaliendelea tena huku afisa mmoja mwandamizi katika kituo hicho akisema "sauti ya mapinduzi ya Kiislamu haitanyamazishwa na operesheni ya kijeshi".
Mkutano wa kilele wa G7 wagubikwa na mzozo huu mpya
Na huko nchini Canada, viongozi wa dunia katika mkutano wa kilele wa kundi la nchi saba tajiri kiviwanda za G7 wamekuwa na juhudi za kutafuta njia ya kudhibiti mzozo kati ya Israel na Iran, huku Rais wa Marekani Donald Trump akionya kwamba Tehran inahitaji kuzuia mpango wake wa nyuklia kabla "haijachelewa."
Trump amesema viongozi wa Iran "wangependa kuzungumza" lakini tayari walikuwa na siku 60 kufikia makubaliano kuhusu mpango wake wa nyuklia na walishindwa kufanya hivyo kabla ya mashambulizi ya anga ya Israel kuanza siku nne zilizopita, akisisitizwa kwamba "lazima wafanye makubaliano". Kiongozi huyo ameandika kupitia mitandao ya kijamii akionya kwamba "kila mmoja anapaswa kuondoka mara moja kutoka Tehran".
Rais Donald Trump wa Marekani amelazimika kukatisha mkutano wa kilele wa kundi la nchi saba tajiri kiviwanda G7 unaofanyika nchini Canada, akisema kuwa ataondoka mapema na kurejea Washington, kutokana na hali inayoendelea Mashariki ya Kati.
Canada na viongozi wa Ulaya wanatazamiwa kuandaa taarifa ya pamoja kuhusu mzozo huo, lakini wanadiplomasia wanasema kuwa Trump hajajitolea kuunga mkono tamko hilo la kutaka kupunguzwa kwa uhasama.
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz aliwaambia waandishi wa habari kwamba Ujerumani inapanga kuandaa pendekezo la mwisho la tamko la pamoja kuhusu mzozo huo, ambalo litasisitiza kwamba "Iran lazima kwa hali yoyote isiruhusiwe kupata nyenzo zenye uwezo wa silaha za nyuklia."Trump apendekeza Iran, Israel zinahitaji 'kupigana' kabla ya kupatana
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer naye amesema viongozi wa G7 wana wasiwasi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran lakini pia anaona kuna haja ya "makubaliano ya kupunguza mapigano."
Katika hali isiyo ya kawaida, Japan ambayo ina uhusiano wa kihistoria na Iran na shinikizo kidogo la ndani kuhusiana na Mashariki ya Kati, imekwenda kinyume na washirika wake wa Magharibi kulaani shambulio la Israel, na kusema kwamba "halikubaliki kabisa na la kusikitisha sana."