Netanyahu:Tunataka ushindi wa haraka Gaza
11 Agosti 2025Katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Jerusalem, Netanyahu ameutetea mpango wake kwa kusema, ndio njia bora na ya haraka katika kuvimaliza vita hivyo vilivyodumu kwa zaidi ya miezi 22.
Waziri Mkuu wa Israel ambae anayekosolewa ndani na nje ya Israel ameongeza kusema kwamba mpango wake huo unalenga "kuvunjilia mbali ngome mbili zilizobaki za Hamas katika mji wa Gaza na kwenye kambi za katikati ya mji huo”, lakini pia utawezesha kuanzisha njia salama na maeneo ya hifadhi kwa raia watakaondoka.
"Israel haina budi kumaliza kazi na kuukamilisha ushindi dhidi ya Hamas. Sasa, tumefanya mengi. Tunadhibiti kijeshi takribani asilimia 70 hadi 75 ya Gaza. "
Aliongeza kwamba "bado kuna ngome mbili. Hizi ni mji wa Gaza na kambi za katikati huko Al Mawasi.”
Hata hivyo msemaji wa Hamas aliyapuuzilia mbali matamshi ya Waziri Mkuu Netanyahu akisema ni "mkururo wa uongo".
Licha ya ukosoaji na maoni mseto kutoka kwa wakuu wa kijeshi wa Israel, Netanyahu amesisitiza: "Watashinda vita, kwa msaada wa wengine au bila msaada wao.” na kuongeza "Lengo letu si kukalia Gaza, bali kuanzisha utawala wa kiraia usio na uhusiano na Hamas au Mamlaka ya Palestina.”
Netanyahu pia alizungumza kwa simu na Rais wa Marekani, Donald Trump, kujadili mipango hiyo mipya ya kijeshi.
Israel yamlenga mwandishi wa Al Jazeera
Ndani ya Gaza, shambulio la anga la Israel hapo jana Jumapili limewaua wanahabari watano wa Al Jazeera, akiwemo mwandishi maarufu Anas al-Sharif, kwa mujibu wa kituo hicho chenye makao yake Qatar.
Hii ni sehemu ya mashambulizi yaliyowalenga moja kwa moja waandishi, kulingana na mashirika ya kufuatilia vyombo vya habari takribani wanahabari 200 wameuawa tangu kuzuka kwa vita hivyo 2023.
Jeshi la Israel katika taarifa yake limekiri kumlenga mwandishi al-Sharif likimtaja kama "gaidi" mwenye mafungamano madhubuti na Hamas.
Muungano wa waandishi wa Habari Palestina umelaani vikali shambulio dhidi ya waandishi hao na kulitaja "uhalifu wa umwagaji damu". Katibu wa Jumuiya ya waandishi wa Habari Palestina amesema huu ni ulengaji wa moja kwa moja wa wavamizi dhidi ya waandishi wa habari wanaotekeleza majukumu yao.
"Kilichotokea ni mauaji mapya yaliyofanywa na Israel inayowakandamiza waandishi wa habari wa Palestina, wamewalenga wafanyakazi wa Al Jazeera pamoja na kundi la wanahabari wenzao waliokuwa wakifanya kazi zao za kitaaluma. Hii inathibitisha kwamba ni mauaji ya kukusudia yanayowalenga watu moja kwa moja."
Itakumbukwa kuwa Israel na Al Jazeera wamekuwa na uhusiano wenye utata kwa miaka chungu mzima, huku mamlaka ya Israel ikipiga marufuku televisheni hiyo kupeperusha matangazo yake nchini humo na kuzivamia ofisi zake kufuatia vita vinavyoendelea vya Gaza.
Mashambulizi ya Israel yamesababisha vifo vya Wapalestina wasiopungua 61,430, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza, takwimu ambazo Umoja wa Mataifa unasema zinaaminika.