Netanyahu: Israel itatwaa maeneo Gaza mateka wasipoachiliwa
26 Machi 2025Akitoa onyo hilo kwa wanamgambo hao Netanyahu amesema, "Tunabadilisha taswira ya Mashariki ya Kati, mapigano yanaendelea Gaza. Kadri Hamas inavyoendelea kukataa kuwaachilia huru mateka wetu, ndivyo tutakavyozidi kuipa shinikizo. Ninasema hivi kwa wenzangu bungeni na ninasema hivi pia kwa Hamas. Hii ni pamoja na kuyachukua maeneo na hatua nyingine ambazo sitazieleza hapa."
Netanyahu ametoa kauli hiyo Jumatano mbele ya Bunge la Israel huku akiutuhumu upinzani nchini mwake kwa kuchochea machafuko baada ya maandamano ya siku za hivi karibuni ya kuipinga serikali yake.
Soma zaidi: Israel yatishia kuiangamiza Hamas ikiwa haitowaachia mateka
Katika hatua nyingine, wanamgambo wa kundi la Hamas wameonya kuwa mateka walio hai wanaoendelea kuwashikilia watauwawa kama Israel itajaribu kuwaokoa kwa nguvu na kuendeleza mashambulizi ya anga kwenye Ukanda wa Gaza. Taarifa iliyotolewa Jumatano na Hamas imesema kundi hilo linafanya kila liwezekanalo ili mateka waendelee kuwa hai, lakini mashambulizi ya Israel yanahatarisha maisha yao.
Israel yatoa amri ya kuwataka wakaazi wa mji wa Gaza kuondoka kwenye makazi yao
Kauli za Israel na Hamas zimetolewa huku kukiwa na taarifa kuwa, jeshi la Israel limetoa amri ya watu kuondoka katika baadhi ya maeneo ya mji wa Gaza wakati likiongeza mashambulizi dhidi ya Hamas.
Juma lililopita, Israel ilianza tena mashambulizi makali ya anga katika Ukanda wa Gaza na kuvunja hali ya utulivu iliyotokana na kusitishwa kwa mapigano na kundi la Hamas mwezi Januari.
Kulingana na wizara ya afya ya Gaza iliyo chini ya Hamas, tangu Israel ilipoanza mashambulizi hayo, takriban Wapalestina 830 wameuwawa.
Nao wanamgambo wa Kipalestina wenye itikadi kali za Kiislamu wa kundi la Islamic Jihad PIJ wamethibitisha kuwa wamefanya mashambulizi ya makombora dhidi ya Israel kutokea Gaza.
Kundi hilo limesema limefanya mashambulizi hayo kujibu uhalifu unaofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina. Kuhusu mashambulizi hayo, jeshi la Israel limesema kombora moja kati ya mawili yaliyorushwa lilizuiwa na jingine liliangukia katika eneo la Zimrat, lililo katika mpaka wa Israel na Ukanda wa Gaza.