Netanyahu awakosoa viongozi wa Uingereza, Ufaransa na Canada
23 Mei 2025Katika ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa X, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema msimamo uliochukuliwa na Waziri Mkuu wa Uingereza na kwa jumla shinikizo kutoka viongozi wa Ufaransa na Canada havitosaidia kupatika amani bali hatua hizo zinalitia shime kundi la Hamas kupigana milele.
Amesema kundi la Hamas limedhamiria kuiangamiza nchi yake na "kuwatokomeza wayahudi wote" na kwamba hailewi ni kwanini Starmer, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney wanapuuza ukweli huo na kuiamuru Israel isitishe operesheni yake Ukanda wa Gaza na hata kutishia kuiwekea nchi hiyo vikwazo.
"Ninamwambia Rais Macron, Waziri Mkuu Carney na Waziri Mkuu Starmer, pale wauaji, wabakaji, waangamizaji watoto na watekaji nyara wanapowashukuru, mjue mko upande usio sahihi wa haki", ameandika Netanyahu kwenye ujumbe huo mrefu ulowalenga viongozi hao watatu walio waungaji mkubwa mkono wa Israel.
Ujumbe huo wa Netanyahu unafuatia ukosoaji wa mapema wiki hii uliotolewa na viongozi hao nchi tatu dhidi ya kile walikitaja kuwa "matendo ya kikatili" ya serikali ya Israel inayotenda kwenye Ukanda wa Gaza.
Mataifa hayo yaliahidi kuchukua hatua iwapo Netanyahu haitobadili mkondo wa operesheni yake ya Gaza.
WFP yasema shehena ya msaada ulioingia Gaza umeanza kusambazwa
Wakati mvutano kati ya Israel na washirika wake ukiendelea, Umoja wa Mataifa umesema umeanza kusambaza msaada wa kiutu uliingia Gaza hivi karibuni ambao ni wa kwanza tangu Israel ilipoweka zuio la kupelekwa mahitaji yoyote Gaza mnamo Machi 2.
Shirika la Msaada wa Chakula WFP limesema ni bekari chache zimeanza tena kufanya kazi na kusambaza mikate.
Hata hivyo Umoja wa Mataifa umekiri msaada huo ambao kwa ujumla ni malori 90 pekee ni kama tone ndani ya bahari. Na hilo linaungwa mkono na waakazi wa Gaza akiwemo Islam Abu Rizk.
"Kila familia inapata paketi moja ya mkate. Bila shaka kifurushi hiki hakitoshi mahitaji ya familia, kwa sababu zipo familia zenye watu watano, wanane hadi kumi. Sasa mfuko huu mdogo hautoshi, kwa sababu (hauletwi) kila siku."
Mnamo siku za karibuni nchi kadhaa zimeelezea wasiwasi mkubwa juu ya hali ya kiutu kwenye Ukanda wa Gaza na hata uamuzi wa Israel wa kutanua kampeni yake ya kijeshi ndani ya ardhi hiyo ndogo ya Wapalestina.
Makumi zaidi wauawa Ukanda wa Gaza kutokana na mashambulizi ya Israel
Katika hatua nyingine, takribani watu 28 wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa kwenye ukanda wa Gaza usiku wa kuamkia leo. Taarifa hizo ni kwa mujibu wa shirika la habari la Kipalestina, WAFA likinukuu vyanzo vya kitabibu.
Israel pia imetoa amri nyingine ya kuwataka watu kuondoka kwenye maeneo kadhaa ya Gaza ambako inapanga kushambulia.
Jeshi la nchi hiyo limesema operesheni dhidi ya kile imekitaja kuwa "mitandao ya kigaidi ndani ya Gaza inafanyika kote kwenye eneo hilo".
Israel inaendelea kukabiliwa na shinikizo la kimataifa. Jumanne wiki hii mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya walikubaliana kupitia upya mkataba wa ushirikiano kati ya kanda hiyo na Israel.
Serikali ya Sweden iliahidi kuushinikiza Umoja wa Ulaya kuwawekea vikwazo mawaziri kadhaa wa Israel na Uingereza ilisitisha majadiliano ya kibiashara na Israel.