Netanyahu awajibu Starmer, Macron na Carney kuhusu Gaza
20 Mei 2025Siku ya Jumatatu, Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, na Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney waliikosoa serikali ya Israel kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi ya kijeshi Gaza, wakionya kuchukua hatua kali ikiwa Netanyahu hatobadilisha mkondo wake.
Hata hivyo, Netanyahu amesema nchi yake itaendelea kushinikiza kuhusu "ushindi kamili" dhidi ya Hamas.
"Tangu mwanzo wa vita tulisema ili kupata ushindi kamili, lazima tuwashinde Hamas na tuwaachie huru mateka wetu wote. Kuna mapigano makali yanayoendelea, mashambulizi mabaya na makubwa. Tutadhibiti sehemu zote za Ukanda wa Gaza, na hilo ndilo tutakalofanya," alisisitiza Netanyahu.
Katika taarifa yao ya pamoja, viongozi hao walisema iwapo Israel haitositisha mashambulizi mapya ya kijeshi na kuondoa vikwazo vyake vya misaada ya kiutu, watachukua hatua Madhubuti zaidi. Viongozi hao pia wameitaka Hamas kuwaachia huru mateka inayowashikilia tangu wakati wa shambulizi la Oktoba 7, 2023.