Netanyahu atishia kuanza mapigano tena Gaza
12 Februari 2025Netanyahu ameyaagiza majeshi yake kujiandaa kuanzisha tena mashambulizi dhidi ya Hamas ikiwa hawatawaachia mateka zaidi siku ya Jumamosi.
"Uamuzi niliopitisha kwa kauli moja katika baraza la mawaziri ni huu: ikiwa Hamas haitawarudisha mateka wetu hadi siku ya Jumamosi mchana, tutasitisha makubaliano ya kusitisha mapigano na Vikosi vya Ulinzi vya Israel vitarejea kwenye mapigano makali hadi tutakapowasambaratisha kabisa Hamas," alisema Netanyahu.
Hamas ilisema siku ya Jumatatu na kurudia jana Jumanne kwamba pengine watasogeza mbele muda wa kuwaachilia mateka watatu wa Israel wakiishutumu kwa kushindwa kukidhi masharti ya makubaliano ya kusitisha mapigano.
Rais Donald Trump wa Marekani baada ya kukutana na Mfalme Abdullah II wa Jordan kwenye Ikulu ya White House jana Jumanne, alielezea mashaka yake ikiwa Hamas watawaachilia mateka wote waliosalia kama ambavyo amekuwa akishinikiza.
Tangu makubaliano hayo yalipoanza kutekelezwa, Hamas imewaachilia mateka 21 na Israel imewaachilia hurur wafungwa 730 wa Kipalestina. Awamu ya pili inataka mateka wote waliosalia kurejeshwa pamoja na makubaliano yasiyo na ukomo ya kusitisha mapigano.