Netanyahu asema wataangamiza viongozi wa usalama wa Iran
17 Juni 2025Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesisitiza hapo jana kwamba kampeni ya Israel dhidi ya Iran "itabadili sura ya Mashariki ya Kati", wakati nchi hizo mbili zikiendelea kushambuliana vikali kwa siku ya tano.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jioni, Netanyahu alisema kuwa Israel inawaondoa viongozi wa kiusalama wa Iran mmoja baada ya mwingine na kwamba kwa kufanya hivyo wanabadili sura ya Mashariki ya Kati, na hilo litaleta mabadiliko makubwa ndani ya Iran yenyewe.
Wakati Netanyahu akitoa matamshi hayo, Iran nayo imeendelea kuvurumusha makombora dhidi ya Israel, huku Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi wa Iran likiapa kuendeleza mashambulizi bila kukatizwa.
Hapo jana pia, Israel ilishambulia jengo la Shirika la Utangazaji la Iran IRIB na kukatiza matangazo ya moja kwa moja. Mtangazaji aliyekuwa hewani alilazimika kukimbia kufuatia mlipuko mkubwa na kusababisha tishio la Iran la kulipiza kisasi dhidi ya vituo vya habari vya Israel.