Kuundwa dola la Wapalestina ni 'kuuzawadia Ugaidi' Netanyahu
15 Aprili 2025Mashambulizi ya Israel leo Jumanne yaliilenga hospitali ya Kuwaiti Field iliyoko ukanda wa Gaza na kumuua daktari mmoja na wengine tisa kujeruhiwa kwa mujibu wa msemaji wa hospitali hiyo. Ni mara nyingine mashambulio yanayolenga hospitali kushuhudiwa baada ya Jumapili kushambuliwa kwa hospitali ya mwisho kubwa Kaskazini mwa Gaza ambayo ilikuwa ikitegemewa kwa huduma muhimu.
Pamoja na Gaza, jeshi la Israel limefanya pia mashambulizi makubwa nchini Lebanon hii leo likisema limemuua kamanda wa kundi la Hezbollah katika shambulio moja la anga lililofanywa karibu na kijiji kimoja cha Kusini mwa Lebanon cha Aitaroun.
Licha ya kufikia makubaliano ya kusitisha vita na kundi la Hezbollah nchini Lebanon,mwezi Novemba mwaka jana,Umoja wa Mataifa unasema raia chungunzima wameendelea kuuliwa tangu wakati huo.
Ofisi ya mkuu wa haki za binadamu wa haki za binadamu imesema kiasi raia 71 wakiwemo wanawake 14 na watoto tisa wameuwawa Lebanon tangu Novemba 27 uliopoanza utekelezaji wa makubaliano hayo ya kusitisha vita. Viongozi mbali mbali wa dunia wamekuwa wakitowa mwito kwa Israel kusitisha vita hivyo vya Gaza na Lebanon.
Hivi leo Emir wa Kuwait Sheikh Meshal al-Ahmad al-Sabah aliyetembelewa na rais wa Misri AbdelFatah al Sisi katika kasri lake la Bayan amesisitiza juu ya ulazima wa kusitishwa vita mara moja katika Ukanda wa Gaza.Soma pia: Hamas yatathmini pendekezo jipya la kusitisha mapigano Gaza
Viongozi wote wawili wametoa msisitizo huo wakisema ipo haja pia ya kuachiliwa huru kwa mateka wa Israel na wafungwa Wakipalestina wanaoshikiliwa kwenye jela za Israel pamoja na kufunguliwa njia ya kupelekwa msaada wa kibinadamu utakaowafikia Wapalestina sambamba na kuanza kwa ujenzi mpya wa Gaza utakaozingatia mpango ulioidhinishwa na mataifa ya Kiarabu na uliopendekezwa na Misri.
Lakini upande mwingine waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekosoa msimamo uliotangazwa na rais Emmanuel Macron wa kutaka kuitambua Palestina kama dola huru katikati ya mwaka huu,akisema kuundwa kwa dola la Wapalestina itakuwa ni sawa na kuuzawadia Ugaidi. Ujumbe huo wa Netanyahu ameutowa baada ya kuzungumza kwa njia ya simu leo na rais Macron.
Hadi tunaiandaa ripoti hii, bado upande wa Palestina ulikuwa haujatowa tamko lolote kuhusu kauli hiyo ya Netanyahu ikiwemo kutoka Mamlaka ya Wapalestina, Ukingo wa Magharibi.Soma pia: Israel yailaumu Lebanon kwa shambulio la makombora, yajibu mapigo
Katika taarifa iliyotolewa baada ya mazungumzo yao Macron hakulizungumzia suala hilo lakini alisisitiza kwamba usitishwaji vita ndio njia pekee ya kuhakikisha kukombolewa kwa mateka waliobakia lakini pia Israel inapaswa kufungua vituo vyote vya ukaguzi kutoa njia kwa misafara ya magari ya msaada wa kibinadamu.
Ndani ya Israel kwenyewe hivi sasa lipo fukuto kubwa la kisiasa, ambako chama cha waziri mkuu Netanyahu cha Likud kimemshutumu mkuu wa shirika la ndani la Ujasusi, Shin Bet-Ronen Bar kwa kuligeuza shirika hilo kuwa chombo binafsi cha mgambo wanawatumikia watu fulani wenye ushawishi kwenye dola.