Ndege ya abiria yagongana na helikopta, Washington
30 Januari 2025Ndege hiyo ilikuwa inakaribia kutua uwanja wa ndege wa Reagan mwendo wa saa tatu usiku kwa saa za Marekani baada ya kupaa kutoka Wichita, Kansas, wakati ajali hiyo ilipotokea.
Tawi la shirika hilo la ndege la Marekani, PSA, inayoendesha ndege hiyo ya abiria ya safari za ndani ya Marekani, imesema kulikuwa na abiria 60 na wafanyakazi wanne kwenye ndege hiyo.
Vyombo vya habari vyaripoti kupatikana kwa takriban miili 18
Vyombo vya habari vya Marekani, vikunukuu vyanzo vya eneo hilo la ajali, vimeripoti kupatikana kwa miili mingi huku shirika la habari la CBS likisema takriban miili ya watu 18 imepatikana.
Wanariadha kadhaa waripotiwa kuwa ndani ya ndege
Gazeti la Washington Post, likinukuu taarifa kutoka kwa baraza la kitaifa linalosimamia mchezo wa kuteleza kwenye theluji likisema kuwa wanariadha kadhaa, makocha na maafisa wake walikuwa ndani ya ndege hiyo.
Afisa mmoja wa Jeshi la Marekani, amesema kuwa helikopta hiyo iliyohusika katika ajali ilikuwa imebeba wanajeshi watatu, lakini vyeo vyao bado havijajulikana kufikia sasa.
Shughuli za utafutaji na uokoaji zinaendelezwa
Shughuli kubwa ya utafutaji na uokoaji inaendelezwa huku wapiga mbizi wakiongeza bidii za kutafuta walionusurika.
Meya wa Washington Muriel Bowser, amewaambia waandishi wa habari kwamba wataendeleza juhudi hizo na kubakia katika eneo la tukio kwa muda utakaohitajika na watajaribu njia zote kuwaokoa ama kutafuta miili ya raia wenzao.
Katika mkutano na waandishi wa habari, mkuu wa idara ya zima moto mjini Washington John Donnelly, amesema kuwa vitengo vya kukabiliana na hali za dharura vyenye takriban maafisa 300, vinaendeleza juhudi za kutafuta na kuokoa waathiriwa wa ajali hiyo chini ya mazingira magumu, lakini hakutoa matumaini yoyote ya kupata manusura.
Trump ashtumu udhibiti wa trafiki ya anga
Katika taarifa rasmi, Rais wa nchin hiyo Donald Trump, amesema amearifiwa kikamilifu kuhusu ajali hiyo na akawaombea kwa Mola waathiriwa wote.
Lakini chini ya masaa manne baada ya mkasa huo na wakati ambapo maafisa wengine wamesisistiza kuwa wanasubiri matokeo ya uchunguzi, Trump alirejea kwenye mitandao ya kijamii kushutumu udhibiti wa trafiki ya anga.
Trump aibua maswali kuhusu ajali ya ndege
Trump amesema ndege hiyo ilikuwa katika mwelekeo mzuri kukaribia uwanja wa ndege, na kuongeza kuwa kwa muda mrefu, helikopta hiyo ilikuwa inaelekea upande wa ndege hiyo, hali iliyomfanya kuhoji kwa nini helikopta hiyo haikupaa juu ama kushuka chini na kwa nini udhibiti wa trafiki ya anga haukutoa mwelekeo kwa helikopta hiyo badala ya kuiuliza kama imeiona ndege hiyo?
Rais huyo alimaliza kwa kusema kuwa ajali hiyo ilikuwa mbaya na ingeweza kuepukika.