Rais wa zamani Ufilipino Duterte ashikiliwa na ICC
13 Machi 2025Mahakama hiyo inatarajiwa katika kipindi cha siku kadhaa zijazo kuanza vikao vya awali vya kesi hiyo,vya kuthibitisha uwepo mahakamani wa mtuhumiwa, kutaja mashataka pamoja na kutangaza tarehe ya kuanza kusikiliza kesi,na kutathmini ikiwa waendesha mashataka wana ushahidi wa kutosha wa kumfungulia kesi kamili.
Soma pia:Rais wa zamani wa Ufilipino Rodrigo Duterte akamatwa kwa warranti wa ICC
Jana mahakama hiyo ilimpokea rais huyo wa zamani wa Ufilipino aliyekamatwa kufuatia warranti wa mahakama hiyo,inayomtuhumu kwa uhalifu wa ubinadamu,kutokana na kampeini aliyoianzisha akiwa madarakani ya kukabiliana na biashara ya madawa ya kulevya, iliyosababisha maelfu kuuliwa nchini Ufilipino.
Awali haikuthibitishwa kwamba amefikishwa ICC
Haikuwa rahisi kuthibitisha iwapo rais wa zamani Rodrigo Duterte bado alikuwepo katika ndege hiyo au la. Baada ya kuwasili Dubai, safari yake ya kuelekea Uholanzi iliahirishwa kwa muda huku baadhi ya waandishi habari wakiripoti kuwa alikuwa akipokea matibabu baada ya video zilizoonekana mitandaoni kumuonesha kiongozi huyo wa zamani akifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na madaktari waliokuwa katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Al Maktoum.
Duterte aliye na miaka 79 alikamatwa baada ICC kutoa waranti wa kukamatwa kwakwe kufuatia tuhuma za kuhusishwa na makosa ya uhalifu wa kibinadamu wakati wa kampeni yake ya kupambana na madawa ya kulevya. Silvestre Bello, moja ya mawakili wake tayari amewasilisha ombi mahakamani akitaka arejeshwe mjini Manila alikokamatwa hapo jana Jumanne (11.03.2025). Bello amesema watakutana haraka iwezekanavyo na timu nzima ya mawakili kujua ni wapi hasa anakopelekwa Duterte na iwapo wataweza kuonana nae.
Rais wa zamani wa Ufilipino Rodrigo Duterte akamatwa kwa warranti wa ICC
Kukamatwa kwa Rodrigo Duterte, aliyewahi kuwa meya na mwendesha mashitaka, aliyeiongoza Ufilipino kuanzia mwaka 2016 hadi 2022, ni hatua moja kubwa katika uchunguzi unaofanywa na ICC, kwa shutuma za uhalifu dhidi ya binaadamu kupitia kampeini yake ya kukabiliana na madawa ya kulevya, iliyosababisha mauaji ya maelfu ya watu hatua iliyokosolewa pakubwa duniani. Duterte atakuwa kiongozi wa kwanza wa zamani wa taifa la bara Asia kufikishwa katika mahakama hiyo ya ICC.
Watoto wa Duterte wawasilisha ombi la kutaka babayao kurejeshwa Ufilipino
Mwanawe wa kike Sara Duterte, ambaye ndie makamu wa rais wa Ufilipino aliabiri ndege kuelekea Uholanzi. Taarifa kutoka ofisi yake haikufafanua ni nini anachokwenda kufanya huko au anapanga kukaa kwa muda gani nchini humo. Mwanawe mwengine wa kike Veronica, anapanga pia kupeleka kesi katika mahakama ya juu ya Ufilipino kuitaka serikali kumrejesha babayake nchini mara moja.
Hata hivyo rais wa sasa wa Ufilipino Ferdinand Marcos Jr aliwaambia waandishi habari hapo jana kwamba ndege iliyombeba mtangulizi wake inaelekea The Hague, ambako anakwenda kujibu mashitaka hayo ya uhalifu wa binaadamu kutokana na kampeini yake ya kupambana na mihadarati.
Kampeni hiyo ndio iliyomuingiza madarakani mwaka 2016 na katika uongozi wake wa miaka sita watu 6,200 waliuwawa wakati wa operesheni ya polisi. Wanaharakati nchini humo wamesema idadi ya waliouwawa inawezekana ikawa kubwa zaidi kutokana na wengi wa waliouwawa kutohusika kwa namna yoyote na biashara ya madawa ya kulevya. Wamesema watu waliuwawa katika hali isiyoeleweka.
afp/reuters