Nchini Iraq wameuawa Waspania na Wajapani.
30 Novemba 2003
TIKRIT:
Wanadiplomasia wawili wa Kijapani waliuawa
iliposhambuliwa gari yao karibu ya mji wa
Tikrit, ukiwa ni mji anakotoka mtawala
aliyepinduliwa wa Iraq, Saddam Hussein. Dereva
wao alijeruhiwa katika shambulio hilo, iliarifu
Wizara ya Mambo ya Nje mjini Tokyo. Waziri wa
Mambo ya Nje, Yoriko Kawaguchi alisema, Japan
haitotishika kabisa katika juhudi zake za
kuupiga vita ugaidi na itaendelea kuchangia
ukarabati wa Iraq. - Kabla ya hapo walipigwa
risasi na kuuawa maajenti saba wa Kispania,
Kusini mwa mji mkuu Baghdad, msafara wao wa
magari uliposhambuliwa kwa makombora ya mkono.
Ajenti wa nane wa Kispania alisalimika baada ya
kujeruhiwa. Waziri wa Mambo ya Ulinzi, Federico
Trillo alisema, maajenti hao waliouawa walikuwa
katika msafara wa magari mawili Kilomita kama
30 Kusini mwa Baghdad. Uspania ni mojawapo wa
washirika wakubwa wa Marekani katika mgogoro wa
Iraq, ikiwa na wanajeshi 1,300 nchini humo.