Nchi za Ulaya kujadili na Iran kuhusu mpango wa Nyuklia
26 Agosti 2025Wajumbe kutoka mataifa ya Ulaya ya kile kinachojulikana kama E3 wanajiandaa leo Jumanne kwa mazungumzo ya dakika za mwisho pamoja na Iran mjini Geneva.
Wajumbe kutoka Uingereza, Ufaransa na Ujerumani wanatarajiwa kujadiliana na Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia, wakati muda wa mwisho uliowekwa na nchi hizo za Ulaya wa kuirudishia vikwazo Tehran ukikaribia.
Mkutano huo wa leo unafuatia mkutano mwingine uliofanyika kabla kati ya mataifa hayo ya Ulaya naIranmjini Istanbul mnamo Julai 25.
Wasiwasi wa nchi za Ulaya kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran umeongezeka tangu nchi hiyo ilipositisha ushirikiano na Shirika la Kudhibiti Nguvu za Atomiki duniani, IAEA, baada ya vita vyake vya siku 12 na Israel, vilivyosababisha kushambuliwa kwa vituo vya nyuklia vya jamhuri hiyo ya Kiislamu ya Iran.