Nchi za kundi la G7 zataka vita visitishwe Sudan
16 Aprili 2025Mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi tajiri kiviwanda duniani za kundi la G7 wametowa mwito wa kusitishwa vita mara moja, bila masharti nchini Sudan.
Mwito huo umetolewa jana, vita hivyo vikitimiza miaka miwili tangu vilipozuka, kati ya jeshi la serikali na wanamgambo wa RSF.
Mawaziri wa G7 na Umoja wa Ulaya wamezitaka pande hizo mbili kukaa kwenye meza ya mazungumzo yatakayoleta tija kumaliza vita hivyo vilivyozuka Aprili mwaka 2023. Tamko la kundi la G7 limetolewa chini ya kiwingu cha mkutano wa kimataifa wa kuisadia Sudan, uliofanyika jana mjini London Uingereza uliowashirikisha wajumbe kutoka mataifa takriban 20 duniani.
Ujerumani ambayo ni miongoni mwa nchi za kundi la G7 iliahidi kutoa dola milioni 142 kwaajili ya kuisadia Sudan na mataifa jirani.
Katika mkutano huo wa London,mashirika mengi ya msaada yamelalamika juu ya kupuuzwa mgogoro huo duniani.