Nchi za Kiarabu zalaani kuzuiwa ziara ya Ukingo wa Magharibi
3 Juni 2025Mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa mengi ya kiarabu waliokuwa wamepanga kuanza ziara leo Jumapili, katika Ukingo wa Magharibi,wamelaani uamuzi wa Israel wa kuzuia ziara hiyo.
Ujumbe wa mawaziri kutoka Saudi Arabia, Misri, Jordan na Bahrain ulipanga kufanya ziara hiyo kwa lengo la kukutana na rais wa mamlaka ya Wapalestina Mahmud Abbas kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Jordan.
Mawaziri hao walitarajiwa kwenye ziara hiyo kuandamana na katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za Kiarabu. Hata hivyo siku ya Ijumaa usiku Israel ilitangaza kwamba haitotowa ushirikiano na kwahivyo kimsingi kuzuia ziara hiyo kwasababu nchi hiyo inadhibiti mipaka ya eneo hilo pamoja na anga.
Afisa mmoja wa Israel alisema rais Mahmoud Abbas alikusudia kuandaa Ramallah mkutano wa kichokozi wa mawaziri wa mambo ya nje kutoka mataifa ya kiarabu, kujadili uungaji mkono wa hatua ya kuundwa dola la Wapalestina.
Aliendelea kusema kwamba Israel haiwezi kutowa ushirikiano katika hatua kama hiyo inayolenga kuidhuru pamoja na usalama wake. Afisa huyo alisema dola la Wapalestina hapana shaka litakuwa ni dola la kigaidi katikati ya ardhi ya Israel.
Endapo ziara hiyo ingefanikiwa kiongozi wa ujumbe huo,mwanamfalme Faisal bin Farhan angekuwa waziri wa kwanza wa mambo ya kigeni wa Saudi Arabia kukanyaga Ukingo wa Magharibi.