Nchi za Kiarabu zaitaka Hamas kuachia madaraka Gaza
30 Julai 2025Mataifa 17 ya Kiarabu, zikiwemo Qatar, Saudi Arabia na Misri, yaliungana pamoja na Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwenye waraka wa kurasa saba kufuatia mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya kuhuishwa kwa suluhisho la mataifa mawili huru kwa ajili ya Waisraeli na Wapalestina ulioandaliwa na Saudi Arabia na Ufaransa.
Sehemu ya tamko hilo lililopewa jina la Tamko la New York ilisema kwamba "kwa muktadha wa kukomesha vita vya Gaza, Hamas lazima isitishe utawala wake Gaza na ikabidhi silaha kwa Mamlaka ya Palestina" kwa msaada na ushiriki wa jumuiya ya kimataifa na kwa lengo la kupatikana kwa dola huru lenye mamlaka kamili la Palestina.
Tamko hilo linafuatia wito uliotolewa mwanzoni mwa mkutano huo na serikali ya Mamlaka ya Palestina ambayo ilizitaka Israel na Hamas kuondoka Gaza na kuiwachia serikali hiyo kuongoza.
Israel imelipinga tamko hilo na hadi sasa Hamas haijatowa msimamo wake.
Uingereza kulitambua taifa la Palestina ikiwa...
Uingereza ilitangaza siku ya Jumanne (Julai 29) azma ya kulitambua taifa huru la Palestina ifikapo mwezi Septemba, kwa kile ambacho Waziri Mkuu Keir Starmer alikiita "hali isiyovumilika kwenye Ukanda wa Gaza."
"Mara zote nimesema tutalitambua taifa la Palestina kama mchango kwa mchakato sahihi wa amani pale utakapowadia wasaa kwa suluhisho la mataifa mawili kuwa la manufaa. Katika wakati suluhisho hilo linahujumiwa, huu ndio wakati wa kuchukua hatua. Kwa hivyo leo kama sehemu ya mchakato huo wa kuelekea amani ninathibitisha kuwa Uingereza itaitambua dola ya Palestina kwenye mkutano wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa mwezi Septemba."
Alisema waziri mkuu huyo wa Uingereza lakini aliongeza kuwa hatua hiyo itachukuwa endapo tu "serikali ya Israel haitochukua hatua madhubiti za kumaliza hali mbaya ya Gaza, kukubali kusitisha mapigano na kuahidi kuunga mkono mchakato wa amani utakaorejesha mezani suluhisho la kuundwa madola mawili."
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amepinga uamuzi huo wa Uingereza, akidai unalizawadia kundi la Hamas, na badala yake ameapa kwamba atafanya kila awezalo kuhakikisha malengo ya Israel yanafikiwa huko Gaza, likiwemo la kuwarejesha mateka nyumbani.
"Nimemaliza mashauriano mengine kuhusu kuachiwa kwa mateka wetu. Tangu ujumbe wetu uliporejea kutoka Qatar, hatujawahi kuacha kujaribu. Kulikuwa na mikutano kila siku, lakini kuna kikwazo kikubwa ambacho kila mtu anakijua: Hamas. Wanaendelea kukataa. Rais Trump, Witkoff, sisi na wapatanishi wote tunalijua hilo. Hatujakata tamaa – tutaendelea kufanya kila tuwezalo kuwarudisha nyumbani." Alisema Netanyahu.
Hatua hiyo ya Starmer inaifanya Uingereza kuwa taifa la pili la Ulaya lililo mwanachama wa kundi la mataifa saba yenye uchumi mkubwa wa viwanda duniani kuongeza mbinyo wake dhidi ya utawala wa Netanyahu.
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa waonya hali mbaya ya njaa Gaza
Wataalamu wanaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa wameonya kuwa hali mbaya kabisa ya njaa inaendelea kujitokeza Gaza, na haitoweza kudhibitiwa iwapo mashirika ya misaada hayatapata fursa ya haraka na isiyo na vikwazo ya kufikisha misaada.
Onyo hilo limetolewa huku mamlaka za afya katika ukanda huo unaodhibitiwa na Hamas zikisema zaidi ya watu 60,000 wameuawa kufuatia mashambulizi ya Israel yaliyoanza baada ya uvamizi wa Hamas wa Oktoba 2023.
Shirika la kimataifa linalofuatilia hali ya upatikanaji wa chakula, IPC, lenye makao mjini Roma lilisema juhudi za kudondosha misaada kutoka angani hazitoshi kuzuia janga la kibinaadamu linaloendelea.
Kwa mujibu wa shirika hilo, endapo hali haikushughulikiwa haraka, basi kitakachoshuhudiwa Gaza vitakuwa vifo vilivyozagaa kila mahala kutokana na njaa.
Ingawa onyo hilo bado halijafikia kiwango cha kuitwa tangazo la baa la njaa, linatokana na ukosoaji mkubwa wa kilimwengu kufuatia kusambaa kwa picha za watoto waliokondeana kabisa na ripoti za vifo kadhaa vinavyotokana na njaa kwenye Ukanda huo baada ya takribani miezi 22 ya vita.
Shinikizo la kimataifa liliifanya Israel kutangaza mwishoni mwa wiki hatua kadhaa za kuruhusu misaada ya kibinaadamu kuingia Gaza, ikiwemo usitishaji wa mashambulizi kwa masaa kumi kwa siku na pia misaada inayodondoshwa kwa njia ya anga.
Lakini Umoja wa Mataifa na Wapalestina wenyewe walioko huko wanasema kuna mabadiliko madogo sana inapolinganishwa na ukubwa wa tatizo la njaa lililopo.