Nchi tatu za Ulaya zatishia kurejesha vikwazo kwa Iran
16 Julai 2025Mabalozi wa nchi hizo tatu katika Umoja wa Mataifa wamekutana siku ya Jumanne ambapo wamejadili uwezekano wa kufikiwa makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran lakini pia uwezekano wa kurejesha vikwazo kwa Iran.
Jambo hilo pia lilizungumzwa kwa njia ya simu siku ya Jumatatu wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alipozungumza na mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa Ujerumani, Ufaransa na Uingereza. Kulingana na maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, mawaziri hao wanne walikubaliana kwamba watahakikisha kuwa Iran haitengenezi na haitapata silaha za nyuklia.
Uingereza, Ufaransa na Ujerumani ni sehemu ya nchi zinazohusika na makubaliano yaliyofikiwa na Iran mwaka 2015 ambayo Rais wa Marekani Donald Trump aliiondoa nchi yake wakati wa muhula wake wa kwanza, akisisitiza kuwa makubaliano hayo yalikuwa dhaifu.
Makubaliano ya mpango wa nyuklia wa Iran ya mwaka 2015
Chini ya makubaliano hayo Iran iliondolewa adhabu za kiuchumi miaka 10 iliyopita kwa kubadilishana na ufuatiliaji wa mpango wake wa nyuklia na kuliwekwa kifungu kinachojulikana kama "snapback" kwa maana kwamba nchi hizo zote tatu za Ulaya kwa pamoja au mojawapo inaweza kurudisha vikwazo vya Umoja wa Mataifa wakati wowote itakapo jiridhisha kwamba Iran haizingatii masharti yaliyowekwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot amesisitiza kipaumbele juu ya hatua ya kuanza tena mazungumzo na kufikiwa makubaliano ya kudumu juu ya mpango wa nyuklia wa Iran.
Kwa upande wake Bunge la Iran limeitaka serikali ya nchi hiyo kukataa kuanza tena mazungumzo na Marekani hadi masharti yake yatimizwe. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema nchi yake itakubali kuanzishwa tena kwa mazungumzo ya nyuklia na Marekani ikiwa tu Iran itahakikishiwa kutoshambuliwa tena baada ya Israel na Marekani kuvishambulia vituo vyake vya nyuklia.
Wakati huo huo Iran imetangaza kuwa imeikamata meli ya kigeni katika Bahari ya Oman kwa tuhuma za kuhusika na ulanguzi wa mafuta. Mojtaba Ghahremani, ambaya ni mkuu wa Mahakama katika jimbo la kusini la Hormozgan amesema meli hiyo ilikamatwa baada ya hati za kisheria zinazohusiana na shehena iliyobeba kupatikana kuwa na mapungufu.
Ghahremani, amesema meli hiyo ilikuwa imepakia lita milioni mbili za mafuta ya magendo na kwamba washukiwa 17, akiwemo nahodha na wafanyakazi wa meli hiyo ya kigeni, wametiwa mbaroni lakini hakufafanua uraia wa waliokamatwa.
Vyanzo: AP/AFP/RTRE