Nchi saba zaihimiza UN kuimarisha kikosi cha usalama Haiti
28 Agosti 2025Mataifa ya Marekani, Canada, na Kenya ni miongoni mwa nchi saba zinazolitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukiimarisha Kikosi maalumu cha Usalama cha kimataifa (MSS) kilichopelekwa Haiti kupambana na magenge ya uhalifu.
Mataifa saba ambayo ni Marekani, Canada, Kenya, El Salvador, Guatemala, Jamaica, na Bahamas yamesema kikosi maalumu cha usalama cha kimataifa kilichopelekwa Haiti kupambana na magenge ya uhalifu hakina uwezo wala rasilimali za kutosha ili kupambana na ghasia zinazooendelea kuongezeka katika nchi hiyo ya Carribean.
Kupitia barua ya pamoja, nchi hizo zimebainisha kuwa zitaunda kikundi cha washirika cha kusimamia ujumbe maalumu ambao awali uliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 2023 ili kuzisaidia mamlaka za Haiti kukabiliana na vurugu na magenge hayo.
Kenya imetuma zaidi ya polisi 700 nchini Haiti
Ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja baada ya kikosi maalumu cha MSS kupelekwa Haiti baada ya juhudi zilizoongozwa na Kenya, hali nchini humo inaendelea kuzorota.
Karibu eneo lote la mji mkuu Port au Prince linadhibitiwa na magenge ya uhalifu. Kati ya maafisa wa polisi 2,500 waliotarajiwa kupelekwa nchini Haiti, ni takriban 1,000 pekee kutoka mataifa sita ndio waliyotumwa, huku Kenya ikiwa imechangia zaidi ya askari 700.
Mwezi Februari mwaka huu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alipendekeza kuundwa kwa ofisi mpya ya Umoja wa Mataifa itakayokuwa na jukumu la kuusaidia ujumbe huo, ambao pia unakabiliwa na ukosefu wa msaada wa kifedha na uhaba wa vifaa.
Aidha Guterres alipendekeza pia kuundwa kwa kundi la washirika wa kudumu litakalokuwa na jukumu la kusimamia mipango ya kimkakati na uratibu wa kikosi hicho, kupata fedha kwa ajili ya wafanyakazi ambao hawatotolewa na ofisi ya Umoja wa Mataifa, pamoja na kuajiri maafisa zaidi wa usalama watakaoshiriki katika kikosi hicho maalum cha usalama cha kimataifa.
Hayo yakiarifiwa, polisi nchini Haiti wamechukua tena udhibiti wa kituo kikuu cha mawasiliano kilichokuwa kimenyakuliwa na magenge ya wahalifu. Michel-Ange Louis Jeune, msemaji wa Polisi ya Haiti amewahakikishia raia kuwa polisi wanaendelea na jukumu la kusimamia usalama.
"Kitendo cha polisi kuchukua tena udhibiti wa kituo kikuu cha mawasiliano, ni ujumbe mzito unaotolewa na kamanda mkuu mpya wa polisi Bw. Andre Jonas Vladimir Paraison. Wakati wananchi wamelala, polisi hawalali. Wanafanya kazi ya kuhakikisha kwamba watu wanaweza kulala bila hofu."
Mapema mwaka huu, shirika la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lilisema kuwa uhalifu wa magenge nchini Haiti umesababisha vifo vya watu 1,500 tangu kuanza kwa mwaka 2025, huku serikali ikionekana kushindwa kukabiliana na vurugu hizo.