Nchi nane zalenga kutoza kodi usafiri wa anga wa kifahari
1 Julai 2025Matangazo
Nchi nane zikiwemo Ufaransa, Kenya, Barbados na Uhispania zimezindua muungano kushinikiza kodi kwa abiria matajiri wa ndege kusaidia nchi masikini kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Hayo ni kwa mujibu wa afisi ya rais wa Ufaransa, ambayo imesema kabla mkutano wa kilele wa mazingira wa Umoja wa Mataifa unaopangwa kufanyika Novemba mwaka huu, muungano wa nchi hizo utashirikiana kuifanya sekta ya usafiri wa anga ichangie zaidi ufadhili wa mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Muungano huo unaozijumuisha pia Somalia, Benin, Sierra Leone na Antigua na Barmuda umesema utafanya juhudi kuongeza idadi ya nchi zinazotoza kodi kwa tiketi za ndege, pamoja na tiketi za abiria wanaosafiri katika kiwango cha biashara na ndege za kibinafsi.