Nchi 9 za EU kusitisha mahusiano ya kibiashara na walowezi
19 Juni 2025Waraka wenye ombi hilo ulitumwa kwa mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas, na kutiwa saini na mawaziri wa mambo ya nje kutoka Ubelgiji, Finland, Ireland, Luxemburg, Poland, Ureno, Slovenia, Uhispania na Sweden. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji Maxime Prevot amesema Ulaya ni lazima ihakikishe uwepo wa sera ya biashara inayoendana na sheria za kimataifa.
Umoja wa UIaya ni mshirika mkubwa zaidi wa biashara wa Israel , ambapo mwaka jana pekee biashara kati ya pande hizo mbili ilifikia thamani ya dola bilioni 48.9, ingawaje haikuwa wazi ni kwa kiwango gani tawala za walowezi wa Israel zilinufaika na biashara hiyo. Viongozi wa Ulaya wanatarajiwa pia kukutana mjini Brussels mnamo Juni 23 ili kujadili muelekeo wa mahusiano yao na Israel.