Nayo Marekani yaipelekea misaada Iran.
28 Desemba 2003WASHINGTON: Nayo Marekani imekwisha pelekea wasaidizi nchini Iran. Msemaji wa Rais George W. Bush alisema, kwamba katika uwiyano pamoja na serikali ya Iran, UM na Shirika la Msalaba Mwekundu serikali imeamua kupeleka misaada ya haraka mjini Bam. Mbali na misaada ya madawa kutoka Marekani, kutoka kituo chake cha kijeshi nchini Kuweit, Marekani imo njiani kupeleka misaada mingine ya vifaa. Nchi hizo mbili hazina mahusiano ya kibalozi tangu 1979 pale ulipovamiwa Ubalozi wa Marekani mjini Teheran na raiya zake 52 kuchukuliwa mateka. Nazo Uswissi, Uingereza, Ucheki, Urusi na Uturuki zimepeleka makundi ya waokowaji maisha. Pia Ujerumani imepeleka wasaidizi 30 kutoka Shirika lake la Misaada ya Kiufundi. Usiku huu huu Ujerumani inadhamiria kupeleka ndege nyingine yenye vifaa vya misaada nchini Iran.